Header Ads Widget

Dk Samia Asema Maboresho ya Viwanja vya Ndege na Ujenzi wa Vituo Vipya vya Utalii Kuimarisha Uchumi

 


Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya usafiri wa anga na utalii, lengo kuu likiwa ni kuimarisha uchumi na kuvutia wageni zaidi nchini.


Akizungumza Oktoba 2, 2025, katika Uwanja wa Sheikh mkoani Arusha mbele ya maelfu ya wananchi, Dk. Samia alibainisha kuwa Kiwanja cha Ndege cha Arusha kimefanyiwa maboresho makubwa yenye thamani ya Shilingi bilioni 17, na mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu.


Kwa maboresho hayo, uwanja huo utaanza kufanya kazi saa 24 kuanzia Januari 2026, hatua itakayosaidia watalii, wafanyabiashara na wakazi wa mkoa huo pamoja na mikoa jirani kupata huduma za usafiri wa anga bila vikwazo.


Aidha, alieleza kuwa kiwanja cha ndege cha Ziwa Manyara, kilichopo Karatu, kimeboreshwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 8.5, ikiwemo ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege yenye lami mita 1,500, jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 150 kwa wakati mmoja, eneo la maegesho ya magari 67 pamoja na barabara ya kuingia uwanjani.


Kuhusu kukuza utalii, Dk. Samia alisema serikali imeimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa ununuzi wa ndege nane katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huku mpango wa kuongeza ndege nyingine nane ukiendelea ili kupanua huduma za shirika hilo ndani na nje ya nchi.


Katika mipango ya muda mrefu, alisema serikali inalenga kuongeza idadi ya watalii kupitia vivutio vipya na miundombinu ya kisasa. Alifafanua kuwa hatua muhimu ni ujenzi wa kituo kipya cha mikutano ya kimataifa jijini Arusha kitakachokuwa na hoteli na miundombinu yote muhimu ya mikutano, ikiwa ni nyongeza ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).


Vilevile, serikali inatarajia kujenga kituo maalum cha urithi wa jiolojia katika eneo la Oldonyo Lengai, Wilaya ya Ngorongoro, kitakachowavutia watalii wanaopenda historia, sayansi na vivutio vya kijiolojia.


Kwa mujibu wa Dk. Samia, miradi hii inalenga sio tu kuongeza idadi ya watalii, bali pia kuchochea biashara, uwekezaji na ajira katika sekta ya huduma na utalii nchini Tanzania.

Post a Comment

0 Comments