Header Ads Widget

Samia Aahidi Hanang Kuwa Kitovu cha Uzalishaji wa Ngano Nchini

 


Hanang, Manyara – Oktoba 3, 2025. Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameweka wazi mkakati mkubwa wa serikali unaolenga kuiwezesha Wilaya ya Hanang mkoani Manyara kuzalisha zaidi ya tani milioni moja za ngano ifikapo mwaka 2030.


Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo, Dk. Samia amesema serikali inatambua uwezo mkubwa wa wakazi wa Hanang katika kilimo cha ngano na mazao mengine, na hivyo imejipanga kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo ili kufikia malengo hayo. Alibainisha kuwa lengo kuu ni kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mahitaji ya ngano kupitia uzalishaji mkubwa unaotarajiwa kutoka Hanang.


Amesema hatua muhimu zitakazochukuliwa ni kushughulikia mashamba makubwa yaliyotolewa kwa wawekezaji lakini hayajaendelezwa. Ameiagiza Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uwekezaji kufanya mapitio ya mikataba na kuona namna mashamba hayo yanaweza kurejeshwa kwa serikali na kugawanywa kwa wakulima wadogo ili kuzalisha mazao kwa tija.


Kuhusu shamba la Basotu, Rais Samia alieleza kuwa serikali itaendelea kulisimamia kupitia Msajili wa Hazina na Halmashauri ya Hanang, huku mwekezaji mpya akisubiriwa. Aidha, aliiagiza halmashauri kuweka gharama za matumizi ya shamba hilo wazi kwa wakulima ili kuondoa mianya ya ulanguzi na vishoka.


Akizungumzia changamoto ya bei ya mbaazi, alisema serikali ipo kwenye majadiliano na India kuhakikisha kuwa bei haitashuka chini ya asilimia 70 ya msimu uliopita. Alifafanua kuwa kushuka na kupanda kwa bei ya mazao ni jambo la kawaida katika biashara, kwani huathiriwa na wingi au upungufu wa bidhaa sokoni.


Ili kuongeza tija ya kilimo, serikali imepanga kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kupitia ujenzi wa bwawa litakalohifadhi maji ya mvua kwa ajili ya mashamba ya Hanang. Sambamba na hilo, alitangaza mpango wa kujenga minara mitano ya mawasiliano katika vijiji vya Sipai, Mogutu, Nalaji, Kisakala na Gidamula ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za mtandao wa simu, akisisitiza kuwa mawasiliano kwa sasa ni nyenzo muhimu ya maendeleo.


Mwisho wa hotuba yake, Rais Samia aliwataka wananchi waende kupiga kura Oktoba 29, 2025 kwa ari na mshikamano, akisisitiza kuwa kura zao ni njia ya kuimarisha heshima ya Chama Cha Mapinduzi.

Post a Comment

0 Comments