Simba Sports Club imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili uliochezwa kwenye Uwanja wa Somhololo, Lobimba.
Ushindi huo unaiweka Simba katika nafasi nzuri kuelekea mchezo wa marudiano utakaochezwa Jumapili ijayo jijini Dar es Salaam, ambapo matokeo chanya yataihakikishia timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Timu hiyo ya Msimbazi iliendeleza rekodi yake nzuri nchini Eswatini, ikiwa imewahi kushinda dhidi ya Manzini Wanderers (1-0) mwaka 1993 na Mbabane Swallows (4-0) mwaka 2018.
Bao la kwanza lilifungwa na Wilson Nangu kwa kichwa dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, baada ya kona safi kutoka kwa Neo Maema.
Bao la pili lilipatikana dakika ya 83 kupitia kwa Kibu Denis, aliyeingia kutokea benchi, akiunganisha pasi ya kisigino kutoka kwa Jonathan Sowah, naye pia aliyeingia kipindi cha pili.
Kibu Denis tena alihitimisha ushindi huo kwa bao la tatu dakika ya 90, akimalizia krosi safi kutoka kwa Morice Abraham.
Katika kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko muhimu kwa kuwaingiza Jonathan Sowah, Kibu Denis, Yusuph Kagoma, Morice Abraham, na Chamou Karabou, wakiwachukua nafasi Wilson Nangu, Charles Ahoua, na Joshua Mutale, hatua iliyoongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.
Kwa upande mwingine, Singida Black Stars imepata matokeo ya kuridhisha katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Flambeau du Centre ya Burundi kwenye Uwanja wa Intwari, Bujumbura.
Bao pekee la Singida lilifungwa na Clatous Chama, ambaye aliibeba timu hiyo na kuhakikisha wanapata matokeo ugenini.
Matokeo haya yanaiweka Singida Black Stars kwenye mazingira mazuri kuelekea mchezo wa marudiano utakaofanyika nyumbani Jumapili ijayo, ambapo ushindi wa aina yoyote au sare tasa (0-0) itatosha kuwapeleka hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
0 Comments