Header Ads Widget

TUNAJUKUMU ZITO LA KUZUIA MAGONJWA ASEMA MGANGA MKUU WA SERIKALI

 


Serikali imesema ina jukumu la kuhakikisha maradhi hayatokei kwa wananchi wake kwa kuendelea kuimarisha huduma za kinga kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 6, 2025 na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe wakati akizungumza na wataalam  (Technical group), kutoka Serikalini, taasisi za kiraia na wadau wa maendeleo wakati akihitimisha warsha ya siku mbili iliyofanyika jijini Dodoma. 

"Uwekezaji Mkubwa uliofanyika na Serikali, lakini uwezeshwaji wa Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii (CHW) ni jitihada za makusudi za kuhakikisha tunawakinga wananchi dhidi ya maradhi yakuambukiza na yasiyo ya kuambukiza," amesema Dkt. Magembe.

Dkt. Magembe amesema zahanati na vituo vya afya vinatakiwa kuwa sehemu ya kueneza elimu ya afya kwa ushirikiano na wahudumu wa afya ngazi ya jamii na ikitokea mtu akapata maradhi basi iwe ni nadra sana.

Dkt. Magembe ameongeza kuwa, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Kanda na Taifa zinatakiwa kujikita zaidi kuwajengea uwezo wataalam waliopo ngazi ya msingi ili mambo mengi yaweze kuishia kwenye ngazi hizo na kupunguza rufaa, aidha hospitali za mikoa, Kanda na Taifa zibakie kwenye huduma maalum pekee. 

Katika hatua nyingine Dkt. Magembe amekitaka kikao hicho cha kitaalam kukutana kila baada ya miezi mitatu ili kuchakata kwa pamoja na kuona wapi kuna changamoto na kuzitatua kwa maslahi ya wanachi.

"Leo tunazungumza tiba utalii,  itakuwa na maana endapo huduma zetu tutaziimarisha kuanzia kwenye ubora tunaojiwekea ikiwepo huduma tunazotoa, muda anaotumia mwananchi kupata huduma lakini kuweka pia mawasiliano yetu , kwa maslahi ya mwananchi, hivyo mnapojadili hakikisheni mnayaweka vizuri haya yote na kuyaleta kwangu kwa hatua zaidi," amehimiza Dkt.Magembe.

Awali akitoa maelekezo ya utangulizi Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya,  Dkt.  Hamadi Nyambea amesema kuwa kikao hicho ambacho kilikaa kwa muda wa zaidi ya miaka 10 iliyopita wameamua kukirejesha ili kupitia na kuangalia sera na miongozo mbalimbali kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa ngazi zote hasa wakizingatia mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sasa.

Post a Comment

0 Comments