Header Ads Widget

Chatanda: “CCM Imeleta Wagombea Wanaokubalika, Tuwaunge Mkono Oktoba 29

 


Mkuranga, Pwani – Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mary Chatanda, amesema chama hicho kimewateua wagombea wanaokubalika na wenye rekodi ya kutekeleza maendeleo, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika Jimbo la Mkuranga, Chatanda alisema jukumu la wananchi sasa ni kutoa kura nyingi za “ndiyo” kwa wagombea wa CCM, kuanzia nafasi ya urais, ubunge hadi udiwani.


Samia Suluhu: Kiongozi wa Miradi na Fursa

Chatanda alisisitiza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amedhihirisha uthubutu wa uongozi kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.


Tukimpa miaka mingine mitano, Dk. Samia ataendelea kufungua fursa za uwekezaji, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha huduma za jamii,” alisema.


Aliongeza kuwa mkoa wa Pwani umenufaika pakubwa kupitia wabunge wake, wengi wao wakiteuliwa kushika nafasi za uwaziri kutokana na uchapakazi wao.


Kura kwa Ulega na Wagombea wa CCM

Akiwaomba wananchi wa Mkuranga kumchagua mgombea ubunge Abdallah Ulega, Chatanda alisema tayari kura za maoni zilionesha imani ya wananchi kwake na sasa ni muda wa kumsaidia kushinda kwa kishindo.


Ndugu zangu, niwaombe tusimame pamoja na Ulega. Tumeonesha mshikamano kupitia kura za maoni, sasa ni wakati wa kuhakikisha tunampigia kura za ushindi,” alisema Chatanda.


Ujumbe kwa Wananchi Kuhusu Mitandao ya Kijamii

Chatanda pia aliwataka wananchi kupuuza taarifa zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii, na badala yake kuzingatia ajenda za maendeleo zinazotekelezwa na CCM.


Katika mkutano huo, viongozi wengine akiwemo Mariam Ulega, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, na Mariam Ditopile, Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, walisisitiza mshikamano wa wananchi kumpigia kura Dk. Samia na wagombea wote wa CCM.

Post a Comment

0 Comments