Header Ads Widget

Ulega: “Katiba Mpya Inahitaji Ushindi wa Dk. Samia Suluhu Hassan

 



Mkuranga, Pwani – Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Alhaj Abdallah Ulega, amewataka Watanzania kuhakikisha wanampigia kura Dk. Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 iwapo wanataka kufanikisha mchakato wa katiba mpya.


Ulega alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni za jimbo hilo, akisisitiza kuwa Rais Samia ni kiongozi wa maridhiano na mwenye dhamira ya kweli katika kutekeleza ahadi zake.

“Dk. Samia ameshatamka wazi kuwa ndani ya siku 100 za mwanzo baada ya uchaguzi, atafufua upya mchakato wa katiba mpya. Kwa hiyo, kura zetu kwake ndizo zitakazowezesha jambo hili kufanyika,” alisema Ulega.


Maendeleo ya Mkuranga na Ahadi Mpya

Mbali na katiba mpya, Ulega ambaye pia ni Waziri wa Mifugo, aligusia uboreshaji wa miundombinu katika eneo hilo, ikiwemo upanuzi wa barabara ya Kilwa kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe, mradi ambao tayari umeanza kutekelezwa ili kurahisisha usafiri na kukuza uchumi wa wananchi.


Aidha, alibainisha kuwa akipata ridhaa ya wananchi, atamshauri Rais kupandisha hadhi ya Wilaya ya Mkuranga kuwa Halmashauri ya Manispaa, kutokana na kasi kubwa ya uwekezaji na ukuaji wa viwanda.

Kwa mujibu wa Ulega, Mkuranga kwa sasa inajivunia zaidi ya viwanda vidogo 100 na viwanda vikubwa 70, hali inayofanya eneo hilo kustahili hadhi ya Manispaa.


Amani na Maendeleo

Akiwaomba wananchi kumpa kura za kutosha yeye na madiwani wa CCM, Ulega alisisitiza kuwa kampeni zao zitakuwa za kistaarabu, wakipita kata kwa kata kumnadi Dk. Samia.


Aidha, aliwakumbusha wananchi kuwa amani ya Taifa ndiyo msingi wa maendeleo:

Pasipo amani hatuwezi kuzungumzia barabara, maji, viwanda, ajira au maendeleo yoyote. Ndiyo maana tunawaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa letu.”

Post a Comment

0 Comments