Header Ads Widget

Dk. Samia Aahidi Kuendeleza Huduma za Kijamii Mtwara

 


Mtwara, Septemba 25, 2025 – Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta za kijamii mkoani Mtwara katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huku akiahidi kuendeleza kasi hiyo iwapo atapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi.


Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Sabasaba, Mtwara Mjini, Dk. Samia alitaja mafanikio yaliyopatikana likiwemo uzinduzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini mwaka 2023, ambayo inatoa huduma za kibingwa kwa wakazi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.


> “Mtwara sasa ina hospitali mbili za rufaa – Ligula na Ndanda – pamoja na hospitali tatu za halmashauri. Serikali itaendelea kupeleka vifaa tiba na kuongeza watumishi wa afya ili huduma ziwe bora zaidi,” alisema.


Miradi ya maji

Dk. Samia alisema serikali tayari imetumia Sh bilioni 87 kutekeleza miradi ya maji katika mkoa huo na kuahidi kukamilisha mradi wa Makonde unaolenga kusambaza maji kutoka Mto Ruvuma.


“Mradi huu ukikamilika utamaliza changamoto ya maji safi kwa wakazi wa Nanyamba, Mtwara Mjini na vijijini,” alisisitiza.


Elimu na ajira za walimu

Akizungumzia sekta ya elimu, Dk. Samia alibainisha dhamira ya Serikali kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kujenga miundombinu, kutoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuongeza ajira za walimu.


> “Tunataka watoto wasome kwenye mazingira mazuri na walimu wawe na nyenzo zote muhimu,” alisema huku akiahidi pia kukabiliana na changamoto ya uhaba wa nyumba za walimu.


Teknolojia na tamaduni

Kwa upande mwingine, mgombea huyo alisisitiza mpango wa Serikali kuhakikisha matumizi ya teknolojia ya kisasa yanaimarishwa katika miaka mitano ijayo, sambamba na kulinda na kudumisha mila na tamaduni za taifa.


Wananchi wasifu maendeleo

Baadhi ya wananchi waliozungumza baada ya mkutano huo walisema wameguswa moja kwa moja na jitihada za serikali ya Dk. Samia, hususan upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima wa korosho na maboresho ya huduma za kijamii.


“Kwa Mkoa wa Mtwara tunajivunia uongozi wa Rais Dk. Samia, ameleta maendeleo makubwa. Oktoba 29 tutampigia kura ya heshima ili ashinde kwa kishindo,” walisema wananchi.

Post a Comment

0 Comments