Header Ads Widget

Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi Arejea Unguja Kufuatia Msiba wa Kaka Yake

 


Unguja, Zanzibar — Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amerejea Unguja mapema leo asubuhi akitokea Pemba, kufuatia taarifa za msiba wa kaka yake, Kapteni Abbas Ali Mwinyi.


Kapteni Abbas, ambaye pia aliwahi kuwa mbunge na rubani maarufu, alifariki dunia Septemba 25, 2025, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Lumumba, Unguja. Marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho, Ijumaa Septemba 26, 2025, katika kijiji chao cha Mangapwani, mara baada ya sala ya Ijumaa.


Taarifa zinaeleza kuwa Dk. Mwinyi alipokea habari za kifo cha kaka yake akiwa kisiwani Pemba kwa ajili ya shughuli za kampeni na majukumu ya kiserikali, jambo lililomlazimu kusitisha ratiba yake na kurejea Unguja mara moja.


Katika kipindi hicho, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alimwakilisha Dk. Mwinyi kwenye hafla ya makabidhiano ya mkandarasi kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pemba na barabara ya Chake–Mkoani.


Msiba huu umeacha simanzi kubwa kwa familia ya Rais Mwinyi na wananchi kwa ujumla, huku viongozi wa kitaifa na wananchi wakitarajiwa kushiriki katika mazishi ya marehemu kesho.

Post a Comment

0 Comments