Header Ads Widget

Dk. Samia: Teknolojia ya Kisasa Kuimarisha Kilimo na Huduma za Jamii

 


Mtwara, Septemba 25, 2025 – Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali ijayo itaongeza kasi ya matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo akili bandia (AI) ili kuongeza ufanisi katika kilimo, huduma za jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.


Akihitimisha kampeni zake mkoani Mtwara, Dk. Samia alibainisha kuwa teknolojia itatumika kwa njia shirikishi na yenye kulinda mila na desturi za Kitanzania.


> “Katika miaka mitano ijayo Serikali inakwenda kufundisha teknolojia ambayo haitafuta, haitaharibu na haitawapotosha vijana wetu wakakiuka mila na desturi zetu. Tunataka teknolojia iwe chombo cha kuijenga jamii, siyo kuibomoa,” alisema.


Teknolojia katika Kilimo

Dk. Samia alieleza kuwa sekta ya kilimo tayari imeanza kunufaika na teknolojia za kisasa, ikiwemo tafiti za udongo, mbegu na uzalishaji bora.


Alitaja uwekezaji katika maabara za kitaalamu, ikiwemo maabara aliyoifungua Julai 2025 kwa ajili ya tafiti na ile ya mwaka 2024 katika Chuo Kikuu cha Sokoine, ambazo zinawafundisha vijana kuzalisha kwa kutumia mbinu za kitaalamu.


> “Tunakwenda pia kuweka vituo vya zana za kilimo ili wakulima wapate huduma kwa bei nafuu na kutumia teknolojia za kisasa shambani,” alisema.


Vipimo na Masoko ya Mazao

Rais huyo pia alieleza jinsi teknolojia inavyotumika kuboresha mifumo ya vipimo na minada ya mazao.


Alisema NFRA sasa inatumia mizani na mifumo ya kisasa kupima unyevu na uzito wa mazao huku wakulima wakipokea taarifa na risiti papo hapo kupitia simu zao.


Aidha, minada ya korosho sasa inafanyika kwa uwazi zaidi kupitia mfumo wa kidijitali unaowawezesha wanunuzi kushindana kwa bei bila kujali umbali.


Maendeleo ya Teknolojia kwa Vijana

Dk. Samia alisema moja ya vipaumbele ni kuhakikisha vijana wanapewa elimu ya teknolojia mashuleni ili waweze kuitumia ipasavyo katika maisha na kazi zao.


> “Teknolojia hii ndiyo inakwenda kufundishwa mashuleni na vijana wetu watakwenda kuitumia kwa kuzingatia mila, tamaduni na desturi za taifa letu,” alisisitiza.

Post a Comment

0 Comments