Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameweka wazi sababu zinazolifanya chama chake kuendelea kufanya kampeni kwa kasi kubwa, hata wakati ambapo baadhi ya watu wanahoji uwepo mdogo wa upinzani kwenye uchaguzi.
Akizungumza na maelfu ya wananchi wa Mlowa, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Dk. Samia alisema kuwa CCM haiwezi kudharau changamoto yoyote, iwe kubwa au ndogo, kwani hata mwiba mdogo unapoweza kuumiza unahitaji kushughulikiwa mapema.
Wapo wanaosema kwa nini mama (Rais Samia) anatumia nguvu wakati hakuna upinzani? Waswahili husema, anayebezwa na mwiba, akimchoma mguu huota tende. Hivyo, kila hali lazima ichukuliwe kwa umakini, ndiyo maana tupo kuomba kura kwa heshima na taadhima,” alisema.
Rais Samia alisisitiza kuwa nguvu ya kampeni za CCM si ya hofu bali ni ishara ya uwajibikaji na heshima kwa wananchi. Alibainisha kuwa kila kura ni muhimu, si kwa urais pekee bali pia kwa wabunge na madiwani, kwani chama kinahitaji mshikamo ili kutekeleza ahadi zake kwa ufanisi.
Aidha, Dk. Samia alieleza kuwa umati mkubwa wa wananchi unaojitokeza kwenye mikutano ya CCM ni kielelezo cha kuridhika kwao na kazi zilizotekelezwa na Serikali yake katika kipindi cha miaka iliyopita.
Hili ndilo jawabu kubwa. Wananchi wameona miradi na huduma zinazogusa maisha yao, ndiyo maana kila sehemu tunapopita tunakutana na umati usio wa kawaida. Hii ni heshima kubwa na ndiyo sababu tunaendelea kuomba kura kwa imani na ujasiri,” aliongeza.
Katika hotuba yake, Rais Samia alibainisha kuwa anatambua wajibu wake kama mlezi wa taifa, akisisitiza kuwa kama mama, ataendelea kulinda maslahi ya Watanzania wote, wakiwemo vijana na watoto, kwa kuzingatia mustakabali wa vizazi vijavyo.
Nina wajibu kama mama mlezi. Watoto wangu ni Watanzania wote. Lazima tuweke msingi thabiti wa maendeleo ili kila mmoja apate nafasi ya kunufaika na rasilimali za taifa,” alisema.
Dk. Samia alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa Chamwino, Iringa na maeneo mengine kote nchini kujitokeza kwa wingi kumpigia kura yeye, wabunge na madiwani kupitia CCM, akiahidi kuwa Serikali itakayoundwa itaendeleza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa yenye kugusa maisha ya wananchi.

0 Comments