Header Ads Widget

DCEA Yadhibiti Nguvu ya Mihadarati: Zaidi ya Kilo 33,000 Zakamatwa, Mitandao Haramu Yavunjwa

 


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imetoa ripoti mpya inayoonesha mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya mihadarati nchini Tanzania. Taarifa hiyo imesema kuwa jumla ya kilo 33,077.623 za dawa za kulevya aina mbalimbali zimekamatwa, huku watuhumiwa 940 wakikamatwa kwa kuhusishwa na matukio tofauti ya biashara hiyo haramu.


Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Septemba 8, 2025, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema kuwa mbali na dawa hizo, mamlaka pia imekamata kilo 4,553 za mbegu za bangi, silaha mbili za moto, magari tisa, pikipiki 26 na bajaji mbili zilizokuwa zikihusiana na uhalifu huo. Aidha, ekari 64 za mashamba ya bangi zimeteketezwa.


Katika moja ya operesheni jijini Dar es Salaam, mtaa wa Tupendane, Manzese, walikamatwa watu watatu akiwemo raia wa Lebanon wakiwa na kilo 2.443 za Cocaine. Dawa hizo ziliingizwa nchini kutoka Brazil kupitia Kenya na Uganda, zikitumika mbinu ya kumezwa na kufikishwa Tanzania kupitia vipenyo visivyo rasmi.


Pia, DCEA ilikamata sigara za kielektroniki 50 zenye bangi, zikiwa zimeingizwa kutoka Uingereza kupitia klabu maarufu za burudani jijini Dar es Salaam. Sigara hizo zilikuwa na kemikali hatarishi kama THC, benzene, cadmium, lead na mekyuri ambazo zina madhara makubwa kiafya ikiwemo saratani na matatizo ya akili.


Katika eneo la Bahari Beach, Dar es Salaam, raia wa Marekani na mkewe raia wa Tanzania walinaswa na chupa 11 za Ketamine pamoja na bangi, na hatua za kisheria zinaendelea dhidi yao.


Vilevile, kupitia kampuni za vifurushi, watuhumiwa wanne walinaswa wakijaribu kusafirisha kilo 10.37 za mirungi kwenda nje ya nchi kwa kuificha kwenye maboksi ya chai. Katika hatua nyingine, mamlaka ilizuia uingizwaji wa lita 69.8 za kemikali bashirifu (MEK na Ephedrine) zilizolengwa kutumika kwenye utengenezaji wa mihadarati.


Mkoani Mara, kinara wa bangi Masero Ryoba Muhabe (44) alinaswa na tani 6.5 za bangi, wakati mkoani humo pia Simoni Gervas Mkonda (51) alikamatwa na kilo 193 za bangi na bastola yenye risasi 11.


Katika mkoa wa Mbeya, Henry Shao (36) na Veronika Samumba (31) walibainika kutengeneza biskuti 241 za bangi kwa kutumia vifaa maalumu, ambapo wateja wao walikuwa wahandisi na vijana wa vyuo.


Kwa upande mwingine, jijini Mwanza, gari aina ya Scania lililokuwa mali ya kampuni ya Coca-Cola Nyanza lilikamatwa likisafirisha kilo 452 za bangi.


Jumla ya kilo 25,919.8 za dawa za kulevya zilikamatwa kupitia operesheni katika mikoa ya Mara, Tabora, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Tanga, Ruvuma na Morogoro.


Kamishna Jenerali Lyimo alisisitiza kuwa DCEA itaendelea kuvunja mitandao ya mihadarati na kufuatilia mbinu mpya zinazotumiwa na walanguzi. Aliongeza kuwa mamlaka itaendeleza utoaji elimu kwa jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya ili kulinda afya, utu na mustakabali wa Taifa.


Post a Comment

0 Comments