Header Ads Widget

Gombo Samandito Aahidi Umeme Bure kwa Kila Nyumba na Huduma za Afya Bila Malipo

 


Mwanza – Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo, ameahidi mageuzi makubwa endapo atapewa ridhaa ya kuongoza nchi, ikiwemo kuhakikisha kila kaya nchini inaunganishwa na umeme bure bila malipo ya awali.


Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kijiji cha Kanyala, Kata ya Bhulyaheke, Wilayani Buchosa mkoani Mwanza, Gombo alisema sera hiyo inalenga kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi na kuimarisha ustawi wa jamii.


Umeme Bila Malipo ya Awali

Akiwahutubia mamia ya wananchi, Gombo alieleza kuwa Tanesco ni shirika la umma linaloendeshwa kwa kodi za wananchi, hivyo hakuna sababu ya Watanzania kutozwa fedha nyingi ili kupata huduma ya umeme.


Tanesco atakapokuta nyumba imekamilika, atalazimika kukuletea umeme moja kwa moja bila malipo yoyote. Kazi yako itakuwa ni kufanya waya ndani ya nyumba yako na kisha kuanza kutumia huduma hiyo,” alisema Gombo huku akishangiliwa na wananchi.



Afya Bure kwa Watanzania Wote

Mbali na umeme, Gombo aliwaahidi wananchi kuwa serikali yake itahakikisha huduma za afya zinakuwa bure kwa kila Mtanzania. Alisema hakuna sababu kwa wananchi kulipia huduma muhimu ya afya wakati rasilimali za taifa zinatosha kugharamia sekta hiyo.


Afya ni uhai. Kwa hiyo, huduma hospitalini zitakuwa bure. Hatutaki kuona mtu anakosa matibabu kwa sababu ya fedha,” alisisitiza.


Ajira kwa Vijana na Watumishi wa Umma

Gombo pia alizungumzia changamoto ya ajira, akibainisha kuwa kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa afya na askari polisi, huku vijana wengi wenye elimu wakiendelea kukosa ajira.


Haiwezekani vijana wamesoma wakabaki majumbani bila ajira, wakati sekta muhimu kama afya na usalama zina uhitaji mkubwa wa watumishi. Serikali yangu itahakikisha nafasi zote zinajazwa,” alisema.


Taswira ya Mabadiliko

Kwa sera zake, Gombo Samandito ameibua mjadala mkubwa kwenye siasa za uchaguzi wa 2025, akijipambanua kama kiongozi anayetaka kuondoa gharama zinazowabana wananchi na kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika moja kwa moja na rasilimali za taifa.

Post a Comment

0 Comments