Header Ads Widget

Dk. Samia: Kituo cha SGR na Bandari Kavu Bahi Kufungua Milango ya Uwekezaji na Ajira

 


Dodoma, Tanzania – Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema ujenzi wa kituo cha treni ya mwendo kasi (SGR) pamoja na bandari kavu vitakavyokuwa Wilaya ya Bahi unakwenda kuibadilisha wilaya hiyo na kuleta fursa kubwa za uwekezaji na ajira kwa vijana.


Akihutubia maelfu ya wananchi wa Bahi wakati akiomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu, Dk. Samia alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya pili na ya tatu ya mradi mkubwa wa reli ya kisasa (SGR).


Pia patakuwa na kituo na bandari kavu ambayo inakwenda kuibadilisha Bahi. Kwa sababu kituo cha SGR na bandari kavu vitavutia uwekezaji, biashara na kwa maana hiyo ajira zitakuwa nyingi kwa vijana wetu. Bahi inakwenda kufunguka,” alisema.


Fidia kwa Wananchi

Aidha, Dk. Samia aligusia changamoto za wananchi waliopisha mradi huo wa reli na miradi mingine ya maendeleo, akiahidi kuwa serikali yake inalifanyia uhakiki suala la fidia na kuhakikisha wananchi wote wanalipwa stahiki zao mara baada ya taratibu kukamilika.


Maendeleo ya Miundombinu

Kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Bahi, Rais Samia alisema serikali imejipanga kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya barabara katika kipindi cha miaka mitano ijayo.


Tumejitahidi kwenye barabara na miundombinu ya barabara. Hapa Bahi tumejenga madaraja 9 na barabara za changarawe kilometa 152 ambazo sasa zinapitika muda wote. Lakini nafahamu bado kuna uhitaji wa barabara zaidi kwa kiwango cha changarawe,” aliongeza.


Bahi Kufunguka Kibiashara

Kwa mujibu wa Rais Samia, uwepo wa kituo cha SGR na bandari kavu Bahi kutaiweka wilaya hiyo katika ramani ya kibiashara kitaifa na kimataifa, hatua ambayo itachochea ukuaji wa uchumi na kupanua fursa za vijana na wakazi kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments