Kaduna, Nigeria – Wakulima wa viungo nchini Tanzania wamepata upepo mpya wa maendeleo baada ya kampuni ya Aavishkaar Capital kuwekeza Dola za Marekani milioni 5 katika kampuni ya Horizon Group, kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao na kuyapeleka kwenye viwango vya kimataifa.
Uwekezaji huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakulima 3,000 nchini Tanzania, Nigeria na Madagascar kupitia Horizon Group ambayo inajihusisha na ukusanyaji, uchakataji na usafirishaji wa viungo kama tangawizi, iliki, mdalasini, karafuu, bizari (manjano) na pilipili manga.
Uwekezaji Unaosaidia Mnyororo wa Thamani
Fedha hizo zimetolewa kupitia Mfuko wa Dunia wa Kusaidia Mnyororo wa Ugavi (GSCSF), kwa kushirikiana na Benki ya KfW ya Ujerumani, ikiwa ni uwekezaji wa nne mkubwa barani Afrika. Lengo ni kusaidia Horizon Group kuongeza mtaji, kununua malighafi na kuhakikisha bidhaa zake zinakidhi mahitaji makubwa ya masoko ya kimataifa, hususan Ulaya, Asia na Marekani.
Horizon Group: Kutoka Nigeria Kuijenga Afrika
Horizon Group ilianzishwa mwaka 2006 nchini Nigeria, na tangu 2017 imejikita kwenye viungo kutokana na ushindani mkubwa wa Tanzania, Nigeria na Madagascar katika sekta hiyo. Hali ya hewa na udongo vinavyofaa kwa kilimo cha viungo vimeziwezesha nchi hizi kuwa vinara wa uzalishaji duniani.
Kampuni hiyo inafanya kazi kwa karibu na wakulima, ikiwapatia mafunzo ya kilimo cha ogani, mbinu bora za uchakataji na kuwaunganisha kwenye vikundi vya ushirika ili kupata ithibati ya kimataifa. Hatua hii imeongeza thamani ya mazao na kutoa nafasi ya kupata bei bora sokoni.
Kauli za Viongozi
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Horizon Group, Jomy Antony, alisema:
Tunafurahi kushirikiana na Aavishkaar Capital tunapoanza awamu mpya ya ukuaji. Uzoefu wao katika kukuza biashara na kufungua masoko utatusaidia kuijenga Horizon kuwa kampuni inayoongoza katika uchakataji wa viungo barani Afrika.”
Kwa upande wake, Darren Lobo, Mkurugenzi wa Aavishkaar Capital, alisema:
Timu ya Horizon Group ina uzoefu wa zaidi ya miaka 80 katika sekta ya viungo. Tunafurahia kusaidia kujenga moja ya kampuni kubwa ya viungo Afrika.”
Aidha, Dr. Markus Aschendorf kutoka KfW aliongeza:
Uwekezaji huu unaakisi dhamira ya kuimarisha mnyororo endelevu wa ugavi Afrika na Asia. Ni hatua muhimu katika kukuza uchumi jumuishi na endelevu.”

0 Comments