Akizungumza kwenye mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi na wanachama wa CCM, Dk. Samia alieleza kuwa ziara yake katika wilaya za Tabora, Urambo na Kaliua, imemuwezesha kuona maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali za maisha, ikiwemo afya, elimu, maji, nishati na kilimo.
> "Jana nilitembelea Wilaya ya Kaliua. Mabadiliko ni makubwa sana. Maeneo yote nikipita, maendeleo yanaonekana kwa macho, na sekta zote zimekua," alisema Dk. Samia.
Sekta ya Umeme na Miundombinu:
Dk. Samia alibainisha kuwa tatizo la umeme katika baadhi ya wilaya limepunguzwa baada ya serikali kujenga kituo cha kudhibiti usambazaji wa umeme katika Ziba, wilayani Igunga. Aidha, upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Tabora umefikia asilimia 95, hatua itakayowawezesha wananchi na wafanyabiashara kupata urahisi wa usafirishaji.
Sekta ya Kilimo na Mifugo:
Kuhusu kilimo, Dk. Samia alisisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa ruzuku kwa wakulima kwa mbolea, pembejeo na chanjo za mifugo. Ujenzi na ukarabati wa skimu za kumwagilia utaongeza uzalishaji mara mbili kwa mwaka. Aidha, maboresho ya minada, majosho na skimu za maji kwa wakulima yameanza kufanikishwa.
Miradi Mikubwa ya Kitaifa:
Dk. Samia alibainisha miradi ya kitaifa itakayopita mkoani Tabora, ikiwemo ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga, mradi wa reli ya mwendokasi (SGR) kutoka Makutupora hadi Isaka, na mradi wa maji unaosambaza maji kutoka Ziwa Victoria na miji 28. Miradi hii itafungua fursa za ajira na biashara kwa vijana na wananchi wa Tabora.
> "Tunaahidi kusogeza karibu maji, umeme, kilimo, ufugaji na uvuvi. Miradi ya maendeleo itadumu na itasaidia kila mwananchi kupata huduma za msingi," alisema Dk. Samia.
Dk. Samia alimalizia kwa kuahidi kuwa Serikali ya CCM, iwapo itapata ridhaa ya wananchi, itasonga mbele katika kuboresha maisha ya wananchi wa Tabora, kuhakikisha maendeleo ya kweli yanaonekana katika sekta zote za kijamii na kiuchumi.

0 Comments