Header Ads Widget

Burkina Faso Yafuta Viza kwa Waafrika: Hatua ya Kihistoria ya Kuimarisha Umoja na Biashara

 


Serikali ya Burkina Faso imetangaza kuondoa ada za viza kwa raia wote wa bara la Afrika, katika hatua inayoelezwa kuwa ni ya kuimarisha mshikamano wa Uafrika na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.


Tangazo hilo lilitolewa Alhamisi wakati wa kikao cha baraza la mawaziri lililoongozwa na kiongozi wa kijeshi, Kapteni Ibrahim Traoré. Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana, alisema kuwa uamuzi huo utaanza kutekelezwa mara moja.


Kuanzia sasa, raia yeyote kutoka nchi ya Kiafrika anayetaka kwenda Burkina Faso hatalipa kiasi chochote cha kulipia ada ya viza,” alisema Sana.


Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, kufutwa kwa ada ya viza kunadhihirisha msimamo wa Burkina Faso katika kuendeleza maadili ya Uafrika (Pan-Africanism), pamoja na kukuza ushirikiano wa kikanda. Hatua hiyo pia inalenga kuongeza fursa za utalii na kuimarisha taswira ya taifa hilo kimataifa.


Hata hivyo, raia kutoka nchi za Afrika bado watalazimika kutuma maombi ya viza kwa njia ya mtandaoni kabla ya kusafiri, ambapo maombi yao yatapitiwa na kuidhinishwa na mamlaka husika.


Burkina Faso, taifa la Sahel linalokabiliwa na changamoto kubwa za usalama kutokana na vitisho vya makundi ya waasi, linaongozwa na Kapteni Traoré aliyechukua madaraka mwaka 2022 kupitia mapinduzi ya kijeshi. Licha ya kushindwa kufanikisha kikamilifu ahadi yake ya kurejesha usalama, kiongozi huyo ameendelea kujipatia sifa miongoni mwa wafuasi wa harakati za Uafrika.


Kwa kuondoa ada za viza, Burkina Faso sasa linaungana na mataifa kama Ghana, Rwanda na Kenya ambayo tayari yamepunguza masharti ya kusafiri kwa wageni kutoka Afrika. Wachambuzi wanasema bado haijulikani iwapo hatua hii itaweza kuimarisha taswira ya nchi hiyo kimataifa, hasa wakati ambapo jeshi linakabiliwa na ukosoaji unaoongezeka wa ndani na nje ya nchi.

Post a Comment

0 Comments