Header Ads Widget

Katavi Yalipuka na Hamasa: Dk. Nchimbi Amnadi Rais Samia na Wagombea wa CCM kwa Kura za Kishindo

 


Habari Kamili

MKOA wa Katavi leo umeshuhudia hamasa kubwa ya kisiasa baada ya Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, kuendelea na mikutano ya hadhara ya kampeni akipenyeza ujumbe mzito wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2025–2030.


Akiwasili katika Uwanja wa Maridadi, Mpanda Mjini, Septemba 9, 2025, Dk. Nchimbi alipokelewa kwa shangwe na mamia ya wananchi waliokuwa wakisubiri kwa hamu kumsikiliza. Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa Ilani ya CCM imebuniwa mahsusi kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi, kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa maendeleo ya Taifa katika miaka mitano ijayo.


Baada ya kuzungumza na wananchi wa Mpanda, Balozi Nchimbi pia aliwanadi wagombea wa chama hicho, akiwemo Mbunge wa Mpanda Mjini, Haidary Hemed Sumry, pamoja na wagombea Madiwani wa maeneo mbalimbali ya mkoa huo.


Awali, akiwa katika mkutano wa hadhara Majimoto, Jimbo la Kavuu, Nchimbi alimtambulisha na kumnadi mgombea Ubunge wa jimbo hilo, Laurent Deogratius Luswetula, sambamba na wagombea wa nafasi za udiwani.


Katika mikutano yote, Dk. Nchimbi hakusita kuwaomba wananchi kumpa kura za kishindo Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wagombea wengine wa chama hicho, ifikapo Oktoba 29, 2025.


Tumuunge mkono Rais Samia na chama chetu kwa kura za kishindo ili tuendelee na safari ya maendeleo tuliyoianzisha. Ni kwa mshikamano huu ndipo Tanzania yetu itaendelea kusonga mbele,” alisisitiza Balozi Nchimbi huku akipigiwa makofi na wananchi.


Mikutano hii ya kampeni inaendelea kuonyesha msisimko mkubwa wa kisiasa katika ukanda wa Magharibi mwa Tanzania, ambapo CCM inalenga kuimarisha nguvu zake kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.


Post a Comment

0 Comments