Kigoma, Septemba 24, 2025 – Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umepongezwa kwa mafanikio makubwa ya utendaji baada ya kufikisha thamani ya shilingi trilioni 9.9 katika mwaka wa fedha 2024/25, ikilinganishwa na trilioni 8.3 mwaka uliopita.
Pongezi hizo zilitolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Mary Maganga, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 55 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NSSF uliofanyika mkoani Kigoma.
Mhe. Maganga alisema mafanikio hayo yametokana na usimamizi bora, matumizi ya TEHAMA na udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato. Aliwataka waajiri kuhakikisha michango ya wafanyakazi inawasilishwa kwa wakati kwa kuwa ni takwa la kisheria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema mafanikio hayo yamechangiwa na utekelezaji wa malengo ya mwaka wa fedha 2024/25, hususan katika ukusanyaji wa michango na matumizi ya TEHAMA. Alisema mafanikio hayo pia ni matokeo ya dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Bw. Mshomba alibainisha kuwa NSSF inalenga kuongeza thamani ya Mfuko hadi kufikia trilioni 11.7 katika mwaka wa fedha 2025/26, licha ya changamoto ya baadhi ya waajiri kuchelewa kuwasilisha michango.
Naye Meneja wa NSSF Mkoa wa Kinondoni, Bw. Large Materu, aliahidi kuwa maagizo yaliyotolewa yatafanyiwa kazi, huku akiweka msisitizo katika ubunifu, TEHAMA na usimamizi wa stahiki za wanachama.

0 Comments