Header Ads Widget

Kigoma Yapata Ahadi Mpya: Samia Asema Hakuna Mwananchi Atakayodhulumiwa Fidia


 


Kigoma, Septemba 14, 2025 – Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa Kigoma kuwa fidia kwa waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege italipwa kwa haki, huku akisisitiza kuwa Serikali ya CCM haitamnyang’anya haki mwananchi yeyote.


Kauli hiyo imetolewa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kigoma Mjini, ambapo mgombea ubunge wa jimbo hilo, Clayton Chipando maarufu Baba Levo, aliwasilisha ombi la wananchi kuhusu fidia hizo.


“Tunafanya uhakiki na uchambuzi wa madai yote. Pale tutakapothibitisha thamani halisi ya maeneo yaliyopimwa, wananchi watalipwa bila kuchelewa. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi haidhurumu watu wake,” alisema Dk. Samia akishangiliwa na maelfu ya wananchi.


Mafanikio na Mipango kwa Wafugaji na Wavuvi

Akizungumzia sekta ya mifugo, Rais Samia alieleza kuwa Serikali inaendelea kujenga majosho, mabwawa na vituo vya chanjo kwa mifugo ili kuboresha sekta hiyo. Pia, alisema mpango wa uboreshaji wa machinjio utaendelezwa kwa lengo la kuinua kipato cha wafugaji.


Kwa upande wa uvuvi, Dk. Samia alisema tayari Kigoma imepokea vizimba 26 na boti mbili za kisasa, na kuongeza kuwa Serikali itaendeleza mikopo ya ununuzi wa boti na vizimba zaidi ili kuimarisha upatikanaji wa samaki kwa soko la ndani na nje.


Uwezeshaji wa Wajasiriamali Wadogo

Katika mkutano huo, Dk. Samia alikumbusha ahadi yake ya kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mitaji ya wafanyabiashara wadogo. Pia, alisisitiza kwamba vibanda vya machinga eneo la Kibirizi vitaboreshwa kupitia Wizara ya Uchukuzi sambamba na uendelezaji wa Bandari ya Kigoma.


Utatuzi wa Changamoto za Mazingira

Akijibu hoja za wananchi kuhusu mafuriko katika eneo la Katibuka, Rais Samia alisema tayari Serikali imeanza mchakato wa kutatua tatizo hilo kwa kudhibiti ongezeko la maji kwenye bwawa la Katibuka, ili kuondoa kabisa changamoto za mafuriko zinazowakumba wakazi wa eneo hilo wakati wa masika.


Aidha, kuhusu changamoto ya vivuko kwenye kata tatu za Kigoma ambazo zinategemea Ziwa Tanganyika pekee, aliahidi kuleta kivuko kipya na cha kisasa kitakachokidhi mahitaji ya wananchi kwa usalama na ufanisi.


Kwa ujumla, hotuba ya Dk. Samia Kigoma imeakisi mtazamo wa Serikali yake wa maendeleo jumuishi – kuhakikisha kila sekta ya wananchi wa Kigoma, kuanzia uvuvi, kilimo, biashara hadi miundombinu, inanufaika na uwekezaji unaofanyika.


Post a Comment

0 Comments