Kigoma, Septemba 14, 2025 – Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuibadilisha sura ya Mkoa wa Kigoma kwa miradi mikubwa ya barabara, umeme, viwanda na kilimo cha michikichi ikiwa atapewa ridhaa ya kuongoza kwa muhula mwingine.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi waliofurika uwanja wa Katosho mjini Kigoma, Dk. Samia alisema Serikali itahakikisha vipande vyote vya barabara kuu vilivyosalia, ikiwemo Manyovu hadi mpakani, vinakamilika kwa kiwango cha lami. Aidha, barabara za vijijini ambazo hazipo kwenye mpango wa lami zitajengwa kwa changarawe ili ziweze kupitika misimu yote.
Katika sekta ya nishati, alieleza kuwa mradi wa umeme wa Mto Malagarasi utazalisha megawati 49.5, na msongo wa kilovoti 132 kutoka Malagarasi hadi Kidahwe utasaidia kupeleka nishati hiyo kwenye vijiji na vitongoji vyote vya mkoa huo. “Umeme utakapokuwa wa kutosha, Kigoma itakuwa kitovu cha uwekezaji, mfano tayari kiwanda cha sukari Kasulu kimeajiri watu 500 na kiwanda kikubwa cha saruji kimeanza kuzalisha bidhaa zake,” alisema.
Kuhusu kilimo, Dk. Samia alisisitiza mpango kabambe wa kukuza zao la michikichi kwa kutoa ruzuku ya miche na pembejeo, akibainisha kuwa lengo ni kuongeza malighafi za kutengeneza mafuta ya kupikia. Aliongeza kuwa Serikali inalenga kuanzisha kongani za viwanda kwa vijana ili kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa Kigoma.
“Tunataka Kigoma iwe lango la biashara. Bidhaa zikizalishwa hapa zina soko kubwa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hii ni nafasi ya kipekee kwa wananchi wa Kigoma,” alisema.
Dk. Samia pia aliahidi kuimarisha huduma za kijamii, ikiwemo afya, elimu, maji safi na salama, na kusambaza umeme katika vitongoji vyote, akisisitiza kuwa maendeleo ya Kigoma ni sehemu ya ajenda kuu ya Serikali ya CCM katika miaka mitano ijayo.

0 Comments