Header Ads Widget

Dakika 10 za Baba Levo: Changamoto za Kigoma Zimegeuka Biskuti kwa Uongozi wa Rais Samia

 



Kigoma Mjini, Tanzania – Mgombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Clayton Chipando maarufu Baba Levo, amekamata hisia za wananchi kwa kutumia dakika 10 kuelezea maono yake ya maendeleo ya jimbo hilo na kutoa pongezi kwa mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.


Baba Levo alizungumza mbele ya Rais Samia na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kwa makini, akianza saa 12:20 mchana hadi saa 12:30. Katika dakika hizo, alielezea hatua kwa hatua changamoto zilizokuwa “mfupa mgumu” kwa wananchi wa Kigoma na jinsi Serikali ya Rais Samia ilivyofanikisha suluhisho.


“Kazi ulizozifanya tulikuwa tunaziita mfupa mgumu, lakini kwako zimekuwa biskuti. Mashahidi wa haya ni wananchi wa Kigoma. Upatikanaji wa maji safi na salama umeboreshwa kwa kiasi kikubwa tangu Rais Samia aingie madarakani. Dada zetu walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita mbili kutafuta maji, hali iliyowachosha kimwili na kuwafanya wazeeke kabla ya wakati,” alisema Baba Levo, akisisitiza mshikamano wa Kigoma na Vibe ya maendeleo.


Kuhusu nishati, Baba Levo ameeleza kuwa tatizo la umeme limepatiwa ufumbuzi baada ya mji kuunganishwa na gridi ya Taifa. “Tangu nimezaliwa tumekuwa tukihangaika na majenereta. Leo hii Mama umelizima na umetufungamanisha na umeme wa Taifa,” aliongeza.


Mbali na hayo, Baba Levo ampongeza Rais Samia kwa maboresho yanayoendelea katika Uwanja wa Ndege wa Kigoma, akisema Serikali imeonyesha dhamira ya kweli kwa kuleta wataalamu na vifaa vya kisasa kuhakikisha uboreshaji unaendana na viwango vya kimataifa.


Hata hivyo, Baba Levo hakusahau kuonyesha changamoto zinazobaki, ikiwemo sekta ya barabara, masoko, na fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo. “Mfupa mwingine ni barabara. Vumbi ni tatizo kubwa. Tunaomba barabara ya kilomita 75 ili kurejesha hadhi ya Kigoma Mjini. Tuna imani kuwa huu nao utakuwa biskuti,” alisema.


Aidha, Baba Levo aliomba kujengwa soko la kisasa katika Kata ya Kibirizi na kuboreshwa kwa masoko ya jioni ili kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kufanya biashara kwa heshima na usalama.


Kuhusu mpinzani wake Zitto Kabwe, Baba Levo alionyesha msimamo wake wa ushindi akisema kwa kejeli: “Mtu ninaeshindana naye ni dhaifu sana. Tutampiga saa tano na nusu, tukabidhi asubuhi.”


Aidha, Baba Levo alimuomba Rais Samia kusaidia katika malipo ya fidia ya Sh.bilioni 8 kwa wananchi waliopisha ujenzi wa uwanja wa Ndege, akisisitiza kuwa lengo lake ni kuona wananchi wanalipwa haki yao na kufurahia maendeleo badala ya kusumbuliwa.


Mwisho wa dakika 10 hizo, Baba Levo aliomba kwa dhati: “Yamekuwa yakisema mengi kuhusu mimi, nakuomba Mwenyekiti na mgombea wetu wa urais maombi yetu wana Kigoma. Nataka niwaoneshe Baba Levo anavyopigania maendeleo ya wananchi wa Kigoma Mjini.”

Post a Comment

0 Comments