Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids, ametuma salamu nzito kwa mashabiki wa klabu hiyo akisisitiza kuwa msimu mpya wa 2025/26 hautakuwa wa majaribio, bali ni msimu wa ushindani wa kweli wenye lengo la kubeba mataji makubwa.
Akizungumza mbele ya mashabiki waliomiminika kwa wingi kwenye Tamasha la Simba Day 2025 lililofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Davids alisema:
Msimu uliopita ulikuwa ni msimu wa kujenga msingi, msimu huu ni kwa ajili ya kubeba mataji, msimu wa kushindania mataji.”
Kauli hiyo ililipua shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki, wakipiga kelele na kuonyesha matumaini mapya kwa kikosi kipya cha Simba.
Simba SC, ambao watashiriki tena Ligi Kuu ya NBC na Ligi ya Mabingwa Afrika, wamekamilisha usajili wa wachezaji wapya wenye viwango vya kimataifa na kuimarisha benchi la ufundi, hatua inayodaiwa kuwa nyenzo ya kurejesha hadhi ya klabu hiyo barani Afrika.
Tamasha la Simba Day limeendelea kuthibitisha ukubwa na hadhi ya Simba, si tu kama klabu ya mpira wa miguu, bali pia kama taasisi ya kijamii inayounganisha mamilioni ya mashabiki ndani na nje ya Tanzania.
Kwa kauli ya Davids, mashabiki sasa wana kila sababu ya kuamini kuwa msimu wa 2025/26 ni wa mapambano makali, na matarajio ya kushuhudia Simba ikiweka historia mpya hayajawahi kuwa makubwa hivi.

0 Comments