Dar es Salaam, Septemba 10, 2025 – Tamasha la Simba Day mwaka huu limepambwa kwa upekee na burudani ya msanii maarufu wa Bongo Fleva, Mbosso (Mbwana Yusuf Kilungi), ambaye aligeuza Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa ukumbi wa muziki wa moja kwa moja.
Mbosso, anayejulikana kwa sauti yake laini na nyimbo zenye kugusa hisia, alijitokeza jukwaani kwa mwonekano wa kuvutia na shoo iliyopangwa kitaalamu. Kuanzia midundo ya mapenzi, nyimbo zake maarufu kama Hodari, Nadekezwa, For Your Love hadi nyimbo mpya, zilimfanya kila kona ya uwanja kulipuka kwa shangwe na kelele za mashabiki waliokuwa na jezi nyekundu na nyeupe za Simba SC.
Umati wa mashabiki ulionekana kushindwa kukaa chini muda wote wa onyesho lake, huku wengine wakipiga simu za moja kwa moja, kurekodi video na kuzirusha mitandaoni. Haswa pale alipoimba nyimbo zake zenye maudhui ya mapenzi, sauti ya umati iliungana naye, ikageuza uwanja mzima kuwa kwaya moja kubwa.
Zaidi ya burudani, Mbosso alitumia nafasi hiyo kutoa ujumbe wa mshikamano na mapenzi kwa mashabiki wake na kwa timu ya Simba SC, akisisitiza mshikikano wa michezo na muziki kama nguzo mbili kubwa za kuleta mshikamano wa kijamii.
Kwa kiwango alichokionyesha leo, Mbosso ameendelea kuthibitisha hadhi yake kama mmoja wa wasanii wakubwa wa kizazi hiki, si tu Tanzania bali pia Afrika Mashariki. Onyesho lake limeacha historia na kuongeza thamani ya Simba Day kama jukwaa la michezo na burudani linalounganisha mamilioni ya watu.

0 Comments