Dodoma, Tanzania – Mgombea urais wa Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, ameibuka na ushindi mkubwa baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutoa uamuzi wa kumrejesha rasmi kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Uamuzi huo, uliosomwa muda mfupi uliopita jijini Dodoma na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, umehitimisha shauri lililokuwa limezua mjadala mkubwa kitaifa, baada ya Mpina kuondolewa kwenye mchakato wa kugombea kwa kuzuiwa kurejesha fomu ya uteuzi.
Mahakama Yamrejesha Mpina Ulingoni
Jopo la majaji watatu – Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza – lilisikiliza kwa kina hoja za pande zote na hatimaye kutoa uamuzi kwamba kuondolewa kwa Mpina hakukuwa halali kikatiba.
Shauri hilo liliwasilishwa kwa hati ya dharura na Bodi ya Wadhamini ya ACT Wazalendo kwa kushirikiana na mgombea wao wa urais, wakipinga hatua ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC-TZ) kumzuia kurejesha fomu za uteuzi.
Wafuasi na Viongozi Mashuhuri Washuhudia
Mamia ya wananchi, wakiwemo wafuasi wa ACT Wazalendo na hata wasio wafuasi wa chama hicho, walifurika katika Masijala Kuu ya Dodoma kufuatilia uamuzi huo.
Miongoni mwa waliokuwa mahakamani ni wanasiasa mashuhuri akiwemo kiongozi mkuu wa zamani wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ambaye alionekana akifuatilia kwa makini mwenendo wa shauri hilo.
Baada ya uamuzi kutangazwa, kelele za shangwe na vifijo vilisikika nje ya mahakama huku wafuasi wa Mpina wakishangilia hatua hiyo kama ushindi wa haki na demokrasia.
Hatua Inayofuata
Uamuzi huu sasa unamrejesha rasmi Luhaga Mpina kwenye kinyang’anyiro cha urais kupitia tikiti ya ACT Wazalendo, hatua inayotarajiwa kuongeza joto la kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kwa ACT Wazalendo, ushindi huu wa kisheria ni ishara ya kuimarika kwa nafasi yao kisiasa, huku chama kikitazamia kutumia hukumu hii kujipatia nguvu mpya za kisiasa na kuwahamasisha wapiga kura kote nchini.

0 Comments