Header Ads Widget

Rais Chakwera Akubali Matokeo ya Uchaguzi, Ampongeza Peter Mutharika kwa Ushindi

 


Lilongwe, Malawi – Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera, amekubali kushindwa katika uchaguzi mkuu unaoendelea, na kulitaarifu taifa kuwa anafanya hivyo kwa heshima ya matakwa ya wananchi waliotaka mabadiliko ya serikali.


Akihutubia taifa leo kabla ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo rasmi, Chakwera alitambua wazi kuwa mpinzani wake, Rais wa zamani Peter Mutharika, ameongoza kwa kiwango kikubwa katika matokeo ya awali. Hadi kufikia Jumanne, Mutharika alikuwa amejizolea takribani 66% ya kura, huku Chakwera akibakia na 24%.


"Ninajua kwamba kwa wengi wenu mliopiga kura, matokeo haya ni taswira ya nia yenu ya pamoja ya kuwa na mabadiliko ya serikali, na hivyo ni sawa kukubali kushindwa kutokana na kuheshimu matakwa yenu kama raia," alisema Chakwera.


Aidha, Chakwera alithibitisha kuwa amempigia simu Peter Mutharika na kumpongeza kwa kile alichokiita "ushindi wa kihistoria". Pia alifafanua kuwa, ingawa alifika mahakamani jana kujaribu kuzuia matokeo yasitangazwe, alikubali uamuzi wa mahakama ulioruhusu tume ya uchaguzi kuendelea na mchakato.


Kwa ujumbe wa mshikamano, Chakwera aliwataka Wamalawi wote kubaki na utulivu bila kujali upande wanaouunga mkono.

"Wamalawi, kama mko upande wa kushindwa au kushinda, tafadhali muwe na amani," alihitimisha.

Post a Comment

0 Comments