Dar es Salaam, Tanzania – Klabu ya Simba SC imefanya mabadiliko ya ghafla katika benchi lake la ufundi baada ya kumteua Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Hemed Suleiman ‘Morocco’, kuwa kocha wa muda wa kikosi hicho. Uteuzi huu unafuatia kuvunjwa kwa mkataba na aliyekuwa kocha mkuu, Fadlu Davids, ambaye pamoja na wasaidizi wake amejiunga na Raja Casablanca ya Morocco.
Kwa mujibu wa taarifa ya Simba, Morocco atakiongoza kikosi hicho katika mchezo muhimu wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana, utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Awali, Kocha Msaidizi Selemani Matola ndiye aliyekuwa anatarajiwa kuchukua mikoba ya muda, lakini amezuiwa kutimiza majukumu hayo kutokana na adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo wa kwanza. Hali hiyo imemlazimu Simba kutafuta suluhisho la haraka, na kwa msaada wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Morocco amekubaliwa kujiunga na benchi la ufundi kwa muda.
Kuondoka kwa Davids na wasaidizi wake kumeacha pengo kubwa klabuni, huku mmoja wa wasaidizi hao, Darien Wilken, akiaga kwa ujumbe wa hisia kali kupitia mitandao ya kijamii. Katika ujumbe wake, Wilken aliishukuru Simba na mashabiki wake kwa muda aliokuwa sehemu ya klabu, akieleza kuwa Simba si timu tu, bali ni familia ambayo atabaki kuiheshimu.
Uteuzi wa Morocco unakuja katika wakati nyeti, ambapo matarajio ya mashabiki wa Simba ni kuona timu yao ikiendeleza safari ya kutafuta mafanikio makubwa barani Afrika.

0 Comments