Los Angeles, Marekani – Mwanamuziki nyota wa Pop na mjasiriamali, Rihanna, amejifungua mtoto wake wa tatu, binti, na mpenzi wake rapa A$AP Rocky.
Mtoto huyo amepewa jina la Rocki Irish Mayers, likiwa na uhusiano wa moja kwa moja na jina la kisanii la babake, ila likibadilishwa kwa herufi moja pekee. Rocki alizaliwa Septemba 13, 2025, na Rihanna alitangaza habari hiyo kupitia chapisho la Instagram, akishiriki picha akimshika binti yake pamoja na glovu ndogo za ndondi za waridi.
Wanandoa hao tayari wana wavulana wawili, Riot na RZA, na walitangaza ujauzito huu wa hivi karibuni kwenye Met Gala ya mwaka huu.
Tangazo hilo limepokelewa kwa shangwe kubwa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo chapisho la Rihanna lilipata zaidi ya milioni 5 likes ndani ya saa mbili. Mashabiki wengi walitoa pongezi huku wengine wakisisitiza matarajio ya kusikia mradi mpya wa muziki kutoka kwake.
Wiki chache kabla ya kujifungua, Rihanna – ambaye jina lake halisi ni Robyn Fenty – alisherehekea kumbukizi ya miaka 20 tangu kutoa albamu yake ya kwanza. Hata hivyo, imepita takribani muongo mmoja tangu atoe albamu yake ya mwisho, Anti, huku akijikita zaidi katika biashara.
Mbali na muziki, Rihanna amejiimarisha kama mfanyabiashara bilionea kupitia chapa yake ya urembo Fenty Beauty na kampuni ya mavazi ya ndani Savage X Fenty. Kwa mujibu wa Forbes, nyota huyo mwenye umri wa miaka 37 ana utajiri unaokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 1.
Alipotangaza ujauzito wake kwa mara ya kwanza kwenye zulia la bluu la Met Gala mwezi Mei, Rihanna alivalia vazi lililodhihirisha wazi hatua za mwanzo za ujauzito wake.
> "Ni wakati wa kuwaonyesha watu kile tulichokuwa tukijiandaa nacho," Rihanna aliwaambia waandishi wa habari kwa tabasamu.
Kuzaliwa kwa Rocki kunapanua familia ya Rihanna na A$AP Rocky, ambao sasa wanajulikana si tu kama wanandoa maarufu bali pia kama wazazi wenye ushawishi mkubwa katika muziki, mitindo na biashara duniani.

 
 
 
 
 
 
0 Comments