Iringa – Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameweka wazi dira yake ya kukuza vyama vya ushirika nchini kama sehemu ya msingi wa kuendeleza kilimo na kuwawezesha wakulima.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Iringa katika mkutano wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, Dk. Samia alisema Serikali yake imechukua hatua madhubuti za kufufua na kuimarisha uchumi wa wakulima kupitia ushirika.
“Tumechukua hatua makusudi kufufua na kuimarisha uchumi, ikiwemo kuanzisha benki ya ushirika na kuimarisha usimamizi kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika, lengo ni kuwezesha vyama vya ushirika kupata mahitaji na mitaji nafuu,” alisema.
Dk. Samia alitolea mfano Iringa Farmers Cooperative Union (IFCU), chama kikuu cha ushirika kilichoanzishwa mwaka 1993, ambacho mwaka 2025/26 kinatarajia kusambaza pembejeo na mbolea ya ruzuku kwa wanachama wake.
Amesema hatua hiyo inaonyesha mafanikio makubwa ya vyama vya ushirika nchini, ambapo sasa vinaweza kujiendesha kibiashara, kusambaza pembejeo, kununua mazao ya wakulima na hata kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, amefafanua kuwa Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo imetoa zaidi ya shilingi bilioni moja ili kuwezesha vyama vya ushirika kusimama imara na kutimiza majukumu yake.
“Tunataka vyama vya ushirika vijikite pia kwenye ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao na kutumia Tehama kuongeza uwazi wa mapato na matumizi. Hapo ndipo mkulima ataona thamani ya jasho lake,” aliongeza Dk. Samia.
Kwa mujibu wa mgombea huyo wa CCM, Serikali imejipanga kuhakikisha vyama vya ushirika vinakuwa na viongozi wenye ujuzi, maadili na uwezo wa kuendesha ushirika kwa tija, hatua itakayoongeza mchango wa wakulima katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

0 Comments