Header Ads Widget

Samia Aahidi Kurejesha Hadhi ya Tanga Kama Kitovu cha Viwanda


 

Tanga, Septemba 29, 2025 — Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa Serikali yake itarejesha hadhi ya Mkoa wa Tanga kama mkoa wa viwanda endapo atapewa ridhaa ya kuongoza Taifa katika Uchaguzi Mkuu ujao.


Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Usagara, Dk. Samia alieleza mikakati ya maendeleo kwa miaka mitano ijayo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa yenye urefu wa kilometa 1,108 kutoka Tanga–Arusha hadi Musoma, ambayo itaunganishwa na Bandari ya Tanga.


> “Reli hii itafungua maeneo ya viwanda na madini hivyo kuongeza fursa za ajira ndani ya Mkoa wa Tanga,” alisema Dk. Samia.


Aidha, alibainisha kuwa reli hiyo ni sehemu ya mpango wa kuboresha Bandari ya Tanga, ambayo Serikali imepanga kuifanya kuwa eneo maalum la bohari ya mafuta na gesi, hatua itakayozalisha zaidi ya ajira 2,100 na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.


Kwa mujibu wake, mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga ambao umekamilika kwa asilimia 84, tayari umeleta manufaa makubwa kwa ajira ambapo zaidi ya watu 3,300 wameshanufaika moja kwa moja.


Vilevile, Serikali imepanga kushirikisha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika ujenzi wa barabara ya Handeni–Singida pamoja na upanuzi na ukarabati wa barabara kuu ya Dar es Salaam–Chalinze–Segera–Arusha.


Katika sekta ya viwanda, Dk. Samia alitangaza kuwa Serikali imefanikisha upatikanaji wa wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha magari ya wagonjwa, hatua itakayoongeza ajira na kuboresha huduma za afya.


> “Mtupe kazi, tukafanyekazi tujenge utu wa Mtanzania. Tujenge utu wa mwana Tanga kwa sababu ukiimarisha huduma za maji, afya, elimu na umeme, unaimarisha utu wa Mtanzania,” alisema.


Amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi ndicho chenye dira ya kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi na kuwataka Watanzania kumpa ridhaa ya kuendelea kuliongoza Taifa.


Post a Comment

0 Comments