Header Ads Widget

Mahakama Yaamuru CHADEMA Kuwasilisha Nyaraka Muhimu Katika Kesi ya Mgawanyo wa Rasilimali Zanzibar

 


Dar es Salaam, Septemba 28, 2025 – Mahakama Kuu imetoa siku 14 kwa upande wa Chadema kuwasilisha nyaraka muhimu zikiwemo Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), taarifa za benki na tamko la mali za chama kuanzia mwaka 2019 hadi 2024, ili kusaidia mwenendo wa kesi namba 8323/2025.


Amri hiyo imetolewa jana na Jaji Hamidu Mwanga wakati shauri hilo lilipoitwa kwa uamuzi mdogo. Walalamikaji katika kesi hiyo ni Said Issa Mohamed, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, wakijitambulisha kama wajumbe halali wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema Zanzibar. Wanawakilishwa na mawakili Alvan Fidelis, Dido Simfukwe na Fabian Joseph, huku wajibu maombi wakitetewa na mawakili Hekima Mwasipu na Dk. Rugemeleza Nshala.


Walalamikaji wanadai kuwa Katiba ya chama na Sheria ya Vyama vya Siasa zimekiukwa, hususan kwenye mgawanyo wa rasilimali kati ya Bara na Zanzibar.


Katika uamuzi wake, Jaji Mwanga alisema:

> “Kwa hali hiyo, natoa siku 14 nyaraka hizo ziwasilishwe Mahakamani na upande wa pili wapewe, kisha zipitiwe ndani ya siku 19 za kazi, yaani hadi Oktoba 24, mwaka huu. Baada ya hapo tutakutana kusikiliza mapingamizi yaliyowasilishwa na walalamikiwa.”


Hata hivyo, Jaji alibainisha kuwa mihutasari ya vikao vya chama haiwezi kutolewa, kwa kuwa walalamikaji hawakutaja tarehe mahsusi za vikao husika na pia baadhi yake ni siri za chama.


Shauri hilo limepangwa kuendelea kusikilizwa tena Oktoba 30, 2025.

Hoja za pande mbili

Awali, wakili wa walalamikaji Alvan Fidelis alisisitiza kuwa nyaraka hizo ni za msingi kwani ndizo zitakazoonyesha iwapo mgawanyo wa rasilimali kati ya Bara na Zanzibar ulizingatiwa kwa usawa.


 “Nyaraka ziko mikononi mwa wajibu maombi. Hawajakataa kuwa nazo, bali wamedai kuna amri ya zuio. Lakini zuio hilo ni la kuzitumia, si kuziwasilisha,” alisema.


Kwa upande wake, wakili wa Chadema Hekima Mwasipu alipinga hoja hizo akisema maombi hayana mashiko, kwa kuwa kumbukumbu za vikao vya Kamati Kuu hazina uhusiano wa moja kwa moja na shauri la msingi, na kwamba nyaraka husika zinaweza kupatikana kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa iwapo mahakama itaagiza.


Aidha, Dk. Nshala alidai baadhi ya walalamikaji hawana viapo vinavyowaruhusu kuendelea na shauri, huku akimnyoshea kidole Said Mohamed, akisema si kiongozi tena wa Chadema baada ya uchaguzi wa Januari 21, 2025, na hivyo kujitambulisha kama kiongozi mwandamizi ni kupotosha.

Post a Comment

0 Comments