Kasai, DRC – Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kuanza rasmi kampeni ya chanjo kwa wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele pamoja na watu waliokuwa karibu na wagonjwa wa Ebola katika Jimbo la Kasai, kufuatia mlipuko mpya wa ugonjwa huo uliotangazwa mapema Septemba.
Kwa mujibu wa WHO, dozi za awali 400 za chanjo ya Ervebo Ebola zimewasilishwa katika eneo la Bulape – kitovu cha mlipuko huo – zikichukuliwa kutoka akiba ya dozi 2,000 zilizopo nchini humo. Aidha, Kundi la Kimataifa la Kuratibu Utoaji wa Chanjo limeidhinisha kutumwa kwa dozi 45,000 zaidi ili kuimarisha juhudi za kudhibiti kuenea kwa maambukizi.
Huu ni mlipuko wa kwanza wa Ebola nchini DRC katika kipindi cha miaka mitatu. Taarifa za hivi karibuni kutoka Wizara ya Afya mjini Kinshasa zinaonyesha kuwa hadi sasa kuna visa 32 vinavyoshukiwa, visa 20 vimedhibitishwa, na tayari vifo 16 vimeripotiwa.
Virusi vya Ebola, ambavyo hupatikana asili yake katika misitu minene ya kitropiki ya Congo, husababisha dalili kali ikiwemo homa, maumivu ya mwili, kutapika na kuhara. Tafiti zinaonyesha kuwa virusi hivyo vinaweza kubaki mwilini mwa walionusurika kwa muda mrefu na kuibuka tena baada ya miaka kadhaa.
Patrick Otim, Meneja wa Kanda ya Mpango wa WHO, alisema wiki iliyopita mjini Geneva kuwa:
Kudhibiti mlipuko huu inawezekana, lakini tutakosa fursa endapo hatua hazitachukuliwa kwa kasi. Serikali na washirika wa afya wanapaswa kuongeza mshikamano
WHO imeeleza kuwa hatua ya haraka ya kutoa chanjo ni muhimu ili kulinda si tu jamii, bali pia wafanyakazi wa afya ambao wako kwenye hatari kubwa ya maambukizi.

0 Comments