Mgombea urais kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Luhaga Joelson Mpina, amekumbana na kikwazo kipya baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza rasmi kuondoa jina lake kwenye orodha ya wagombea wa kiti cha urais.
Uamuzi huo umetokana na pingamizi lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Said Johari, dhidi ya uteuzi wa Mpina, likidai hana sifa za kisheria kuendelea na kinyang’anyiro cha urais.
Hatua hii imekuja siku nne pekee baada ya Mpina kushinda kesi Mahakama Kuu – Masjala Kuu ya Dodoma, iliyotengua uamuzi wa awali wa Tume uliokuwa umemzuia kurudisha fomu za uteuzi wake.
Kwa mujibu wa taarifa ya ACT Wazalendo, pingamizi hilo limejengwa juu ya hoja ya uamuzi wa awali wa Msajili wa Vyama vya Siasa, huku chama hicho kikikituhumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuhusika katika kulazimisha kuondolewa kwa jina la Mpina.
“Mapingamizi haya hayana msingi wowote wa kisheria wala ukweli. Ni njama za kisiasa zinazolenga kuzuia mgombea wetu,” chama hicho kilieleza kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Hadi sasa, haijabainika iwapo ACT Wazalendo itachukua hatua nyingine ya kurejea mahakamani kupinga uamuzi huu mpya wa Tume.

0 Comments