Header Ads Widget

Hamisi Mwinjuma ‘MwanaFA’ Aeleza Kazi ya Samia Muheza, Ataka Kura za Kishindo CCM

 


Mbunge wa Jimbo la Muheza, Hamisi Mwinjuma maarufu kama MwanaFA, amewaeleza wananchi wa Kata ya Mkuzi kwamba maendeleo yanayoonekana katika sekta ya afya na maji ni matunda ya juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo kuwataka wapiga kura wasipoteze kura hata moja kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Ameeleza kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, vituo vipya vya afya vimeanzishwa ikiwemo cha Ubwari, ambacho awali kilikuwa na changamoto ya hati ya eneo lakini sasa kimepitishwa rasmi na kimeanza kupata mgao wa huduma. Aidha, kituo cha Bwembera kilichopo Kata ya Kwafungo kimejengwa, huku kituo cha Amani kikipokea zaidi ya shilingi milioni 645 kwa ajili ya ujenzi wake. Vilevile, kituo cha Ngomeni kilichopo Kata ya Misozwe kimepokea shilingi milioni 250 kwa ujenzi.


Kuhusu huduma za maji, Hamisi Mwinjuma (MwanaFA) alibainisha kuwa kiasi cha shilingi milioni 175 kimetumika kwenye miradi ya vijiji vya Mafere, Mkuzi na Mindu. Aliongeza kuwa mradi mkubwa wa miji 28 wenye thamani ya shilingi bilioni 40 utakapokamilika, tatizo la maji Muheza litakuwa historia.


“Nina kimbelembele cha kusimamia mahitaji yenu, lakini fedha na utekelezaji unatolewa na Rais Samia. Hivyo, kura zenu zote lazima ziende CCM,” alisema Mbunge huyo kwa msisitizo.


Katika mkutano huo, mgeni rasmi ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Tanga, Faraha Mvumo, alikabidhi Ilani ya Uchaguzi kwa mgombea udiwani wa Kata ya Mkuzi, Sharifa Kivugo, na kumnadi Mbunge pamoja na mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha dhamira ya chama kuendelea kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli.


Post a Comment

0 Comments