Header Ads Widget

Jeshi la Polisi Latoa Uhakikisho wa Usalama Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025

 

Jeshi la Polisi Tanzania limewahakikishia wananchi na wageni waliopo nchini kuwa hali ya usalama ni tulivu na imara kuelekea siku ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.


Kupitia taarifa iliyotolewa leo, Oktoba 26, 2025, kutoka Makao Makuu ya Polisi jijini Dodoma, msemaji wa Jeshi hilo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi.


DCP Misime alisisitiza kuwa hakuna tishio lolote la kiusalama nchini, licha ya kuwepo kwa taarifa zinazozagaa mitandaoni kuhusu uwepo wa maandamano. Amesema Polisi wamejipanga kikamilifu kulinda usalama wa raia, mali zao na kuhakikisha shughuli zote za uchaguzi zinafanyika kwa utulivu.


Tunaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa zote za kiusalama. Wananchi wasiwe na hofu, wajitokeze kwa wingi kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kwa amani,” amesema DCP Misime.


Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kudumisha amani nchini, huku likionya wale watakaothubutu kuvunja sheria kwa visingizio vya maandamano yasiyoruhusiwa.

Post a Comment

0 Comments