Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha takribani miaka 500, Kanisa la Anglikana limevunja historia yake kwa kumteua Dame Sarah Mullally, mwenye umri wa miaka 63, kuwa Askofu Mkuu Mteule wa Canterbury. Uteuzi huu ni hatua kubwa kwa taasisi hiyo ya kidini ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wanaume.
Dame Sarah Mullally si mgeni katika uongozi na uvumbuzi. Kabla ya kuingia kwenye wito wa kikuhani, alijijengea jina kubwa katika taaluma ya afya. Mwaka 1999 aliweka rekodi kwa kuwa afisa mkuu wa uuguzi mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Uingereza. Baada ya kujiunga na utumishi wa Kanisa, alikua haraka na hatimaye kuhudumu kwa zaidi ya miaka saba kama Askofu wa London, nafasi ambayo ilimfanya kuwa mshiriki wa tatu kwa ukubwa miongoni mwa makasisi wa Anglikana na mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.
Hata hivyo, safari yake haikuwa rahisi. Wanawake waliruhusiwa kuingia rasmi katika utumishi wa upadre wa Kanisa la Anglikana katikati ya miaka ya 1990. Hadi sasa, bado kuna upinzani mkubwa kutoka kwa baadhi ya maaskofu wakuu ndani ya Kanisa wanaopinga vikali wazo la wanawake kuwa mapadri, sembuse kuongoza taasisi hiyo kubwa. Pamoja na changamoto hizo, uteuzi wa Dame Sarah unatazamwa kama ushindi wa kihistoria kwa usawa wa kijinsia na ishara ya mabadiliko ya taratibu katika taasisi za kidini zenye mizizi ya kale.
Sheria za Kanisa zinawataka Maaskofu Wakuu wa Canterbury kustaafu wanapofikisha miaka 70, jambo ambalo lilifanya wengi kuamini kwamba umri wa Dame Sarah ungekuwa kikwazo kwake kuteuliwa. Hata hivyo, uteuzi huu umevunja matarajio hayo na kuonesha dhamira ya Kanisa kufungua ukurasa mpya katika historia yake.
Tarehe rasmi ya kutawazwa kwake bado haijatangazwa, lakini bila shaka uteuzi huu tayari umeweka alama kubwa, ukiwa ni kumbukumbu itakayodumu kwenye historia ya Kanisa la Anglikana na jamii pana ya kikristo duniani.
0 Comments