Header Ads Widget

Polisi Watoa Onyo Juu ya Matumizi Mabaya ya Mitandao Kufuatia Video ya “Kapteni Tesha”

 


Dar es Salaam, Oktoba 6, 2025 — Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa onyo kali dhidi ya kile lilichokiita “matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii” kwa kusambaza maudhui yenye viashiria vya uchochezi na uhalifu, kufuatia video inayomuonesha mtu anayejitambulisha kama Kapteni Tesha, anayedai kuwa afisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).


Katika video hiyo yenye muda wa takribani saa moja na dakika ishirini, mwanaume huyo anaonekana akitoa ukosoaji mkali dhidi ya serikali, akitaja masuala ya ufisadi, ushawishi wa kisiasa ndani ya jeshi na ukiukwaji wa haki za binadamu. Aidha, anamtaka Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, kuchukua hatua za kulinda maslahi ya taifa na raia wake.


Taarifa rasmi ya Polisi iliyotolewa Jumapili imesisitiza kuwa maudhui kama hayo yanakiuka sheria za nchi na yanatishia utulivu wa umma.


Tabia hizi lazima zilaaniwe na kupigwa vita na kila Mtanzania anayeuthamini amani ya nchi na familia yake,” imeeleza taarifa hiyo ya Polisi.


Wakati huo huo, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wake, Kanali Bernard Masala Mlunga, limeonya dhidi ya juhudi za watu wanaojaribu kulihusisha jeshi na masuala ya kisiasa kupitia mitandao ya kijamii.


Kanali Mlunga alisema baadhi ya watu hao wanadai uanachama wa jeshi kwa uongo, huku wengine wakiwa ni waliowahi kufukuzwa kazi kwa sababu za utovu wa nidhamu au mienendo ya kisiasa.


Jeshi linaendelea kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kwa uadilifu, uaminifu na weledi kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mlunga.


Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, majaribio ya kuthibitisha utambulisho wa mtu huyo hayakufanikiwa baada ya maafisa wa kijeshi kutojibu maombi ya maoni.


Wanaharakati wa ndani wametumia mitandao ya kijamii kusambaza video hiyo, wakidai kuwa ujumbe wa “Kapteni Tesha” unawakilisha sauti ya wananchi wanaotaka uwazi na haki.


Tukio hili linajiri wakati Tanzania ikiingia kwenye kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika wiki tatu zijazo. Hali ya kisiasa imeendelea kuwa tete baada ya chama kikuu cha upinzani CHADEMA kupigwa marufuku kushiriki uchaguzi, huku mwenyekiti wake Tundu Lissu akibaki rumande akikabiliwa na kesi ya uhaini.

Post a Comment

0 Comments