Sengerema, Mwanza – Oktoba 7, 2025:
Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa rai kwa Watanzania kuliheshimisha Taifa lao ndani na nje ya nchi, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, kutii sheria, na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Tabasamu, wilayani Sengerema, Dk. Samia alisema heshima ya nchi ni kitu cha msingi kinachopaswa kulindwa na kila Mtanzania, bila kujali nafasi yake katika jamii.
Ni wajibu wetu kuheshimisha Taifa ndani ya nchi na nje ya nchi. Tutaheshimisha nchi yetu kwa kuweka amani, kufanya chaguzi bila vurugu, na kufuata sheria pamoja na haki za kila mtu,” alisema Dk. Samia.
Ameongeza kuwa, nje ya mipaka ya Tanzania, heshima ya Jamhuri ya Muungano imejengwa kutokana na diplomasia thabiti ambayo imeifanya nchi kuwa na taswira njema duniani.
Mpaka hatua tuliyofikia, jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni zuri sana na linaheshimika. Serikali yenu ikipata ridhaa, tutaendelea kuimarisha mahusiano yote yanayolenga ustawi wa kijamii na maendeleo ya watu,” alisisitiza.
Aidha, Dk. Samia aliwataka Watanzania kuepuka tabia ya kubeza mafanikio ya nchi, akisema baadhi ya watu wamekuwa wakipinga au kushusha hadhi ya Tanzania kimakusudi.
Wapo Watanzania ambao kila wakiona jina la Tanzania linaheshimika duniani, kazi yao ni kulishusha. Nawaomba tuachane nao, waacheni waende kivyao. Hao siyo wenzetu,” alisema kwa msisitizo.
Katika hotuba hiyo, Dk. Samia pia aliwapongeza wakazi wa Sengerema kwa maandalizi ya uzinduzi wa mgodi mkubwa wa Nyansaka, akisema ni moja ya miradi mikubwa ya madini nchini ambayo itatoa ajira nyingi kwa vijana na fursa za biashara kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Mwanza.
Kuhusu uchaguzi mkuu, mgombea huyo wa CCM aliwahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba kupiga kura kwa amani na kuchagua chama hicho ili kuendeleza utekelezaji wa Ilani ya Maendeleo.
> “Nataka kuwaambia, tumeweza na tutaweza. Mimi mgombea urais, wabunge na madiwani wa CCM tunawaomba mtupatie ridhaa ili tuendelee kuwaletea maendeleo. Nendeni mkapige kura, amsha rafiki yako, familia yako, na majirani zako,” alisema.
Amesema ni muhimu kuwachagua viongozi wa CCM katika ngazi zote ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unakuwa wa ufanisi bila migongano ya kisera.
Mkiwachanganya, sauti zitagongana. Huyu atasema ndiyo, huyu atasema siyo. Tukachague viongozi wa CCM wote ili maendeleo yasimame kwa nguvu moja,” alihitimisha.
0 Comments