Header Ads Widget

MUSSA AZZAN ZUNGU ACHAGULIWA KUWA SPIKA MPYA WA BUNGE LA 13 TANZANIA

 


Dodoma — Mussa Azzan Zungu amechaguliwa kuwa Spika mpya wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akipata kura 378 kati ya kura 383 zilizopigwa na wabunge katika mkutano wa kwanza wa kikao cha kwanza cha Bunge hilo.


Kwa matokeo hayo, Zungu anakuwa Spika wa nane wa Bunge la Tanzania tangu kuanzishwa kwake, baada ya kuwashinda wagombea wa vyama vingine waliopata jumla ya kura mbili pekee, huku kura tatu zikiharibika.


Zungu, ambaye aliteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania nafasi hiyo, amechukua nafasi ya Dk. Tulia Ackson, aliyekuwa Spika wa Bunge la 12, ambaye alijitoa katika kinyang’anyiro hicho kwa sababu ambazo hazikuelezwa rasmi.


Aidha, Daniel Sillo amechaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge hilo, akitarajiwa kushirikiana na Zungu katika kuongoza shughuli za Bunge kwa kipindi kijacho.


Katika historia ya Bunge la Tanzania, waliowahi kushika wadhifa wa Spika ni Adam Sapi Mkwawa, Erasto Andrew Mbwana Mang’enya, Pius Msekwa, Samuel John Sitta, Anna Makinda, Job Ndugai, na Dk. Tulia Ackson.


Zungu, ambaye pia ni Mbunge wa Ilala (CCM), anatajwa kuwa na uzoefu mkubwa wa kisiasa na wa muda mrefu katika shughuli za Bunge, akitarajiwa kuendeleza misingi ya uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika chombo hicho cha kikatiba.

Post a Comment

0 Comments