Header Ads Widget

MBUNGE MAVUNDE AONGOZA UZINDUZI WA UJENZI WA ZAHANATI YA MASEYA, HOMBOLO MAKULU

 


Dodoma--Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Mheshimiwa Anthony Mavunde, ameungana na mamia ya wananchi wa Mtaa wa Maseya, Kata ya Hombolo Makulu, kuanzisha rasmi ujenzi wa zahanati ya mtaa huo, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Mavunde aliwashukuru wananchi wa Maseya kwa kumuunga mkono yeye, Rais Samia Suluhu Hassan, na Diwani wa kata hiyo kwa kura nyingi wakati wa uchaguzi uliopita.


Kazi yetu sasa ni kutatua changamoto za wananchi. Nawapongeza kwa kujitokeza kwa wingi katika ujenzi wa zahanati yetu, ambayo itasogeza karibu huduma za afya kwa wananchi wa Maseya,” alisema Mavunde.


Mbunge huyo aliahidi kuchangia matofali 2,000 na mifuko 100 ya saruji ili kuhakikisha jengo la zahanati linakamilika hadi hatua ya upauaji, huku akieleza imani yake kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaunga mkono juhudi hizo katika kukamilisha ujenzi huo.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Maseya, Ndugu Alexander Fwalu, alitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa haraka wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo usambazaji wa umeme na uchimbaji wa visima vya umwagiliaji kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.


Fwalu pia alimpongeza Mheshimiwa Mavunde kwa kutimiza ahadi yake ya kuanzisha ujenzi wa zahanati hiyo na kuahidi kuwa wananchi wa Maseya wataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na huduma za afya zinasogezwa karibu zaidi kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments