Dodoma, Novemba 13, 2025 — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo amewasilisha rasmi bungeni jina la Dk. Mwigulu Lameck Nchemba kwa ajili ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Hati ya uteuzi huo iliwasilishwa bungeni jijini Dodoma na Mpambe na Mshauri wa Masuala ya Kijeshi wa Rais, Brigedia Jenerali Nyamburi Mashauri, kwa niaba ya Rais. Hati hiyo, iliyowekwa ndani ya bahasha maalum, ilifunguliwa na Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu, ambaye aliwasilisha taarifa hiyo kwa wabunge kwa mujibu wa Ibara ya 51(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya hatua hiyo, wabunge wanatarajiwa kumpigia kura ya kuthibitisha uteuzi wa Dk. Nchemba kabla ya kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo.
Dk. Mwigulu Nchemba, ambaye ni mchumi kitaaluma na kada wa muda mrefu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwemo Waziri wa Fedha na Mipango katika serikali ya Rais Samia.
Kwa uteuzi huu, Dk. Nchemba anakuwa Waziri Mkuu wa 12 tangu Tanzania ipate uhuru, akimrithi Kassim Majaliwa Majaliwa, anayemaliza muda wake baada ya kulitumikia taifa kwa miaka kadhaa katika nafasi hiyo.

0 Comments