Header Ads Widget

Rais Samia Atangaza Msamaha kwa Vijana Walionaswa Kwenye Maandamano ya Uchaguzi


Dodoma, Tanzania — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza msamaha kwa kundi kubwa la vijana waliokamatwa kufuatia maandamano ya siku tatu yaliyojitokeza kuanzia siku ya uchaguzi, Oktoba 29, 2025. Akizungumza katika ufunguzi wa Bunge la 13, Rais Samia alisema kuwa sehemu kubwa ya vijana hao “walifuata mkumbo” na hawakujua uzito wa vitendo vyao.


Akitumia mamlaka yake kwa mujibu wa Ibara ya 91(1) ya Katiba, Rais Samia alielekeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuchunguza upya mashitaka yao, hususani yale ya uhaini, na kuwaachia wale ambao hawakuwa na nia ya kufanya uhalifu.


Rais alisema kuwa vijana wengi waliojipata katika vurugu hizo wanapaswa kurejeshwa kwa familia zao ili kuendelea na maisha, huku akisisitiza kuwa taifa linahitaji malezi na mwongozo kwa vijana badala ya kuwaadhibu bila sababu za msingi.


Maandamano hayo yaligharimu maisha ya watu kadhaa, kusababisha majeruhi, na kuharibu mali za umma na binafsi tukio lililosababisha zaidi ya vijana 600 kukamatwa na kufunguliwa mashtaka mazito.


Katika hotuba yake, Rais Samia alitoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao na kueleza masikitiko yake kuhusu tukio hilo. Aliwaomba wabunge na wageni waalikwa kusimama kwa dakika moja kuwaombea marehemu.


Akitangaza hatua zaidi, Rais alisema serikali imeunda tume maalum kuchunguza undani wa matukio yaliyotokea wakati wa maandamano. Matokeo ya uchunguzi huo yanatarajiwa kuongoza hatua za maridhiano na kurejesha utulivu katika taifa.


Akiwasisitizia vijana, Rais Samia alikumbusha kuwa Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, umoja na maelewano, na akaitaka jamii kulinda misingi hiyo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.


Post a Comment

0 Comments