Header Ads Widget

WAKATI MAONESHO YA NANENANE YAKIENDELEA WANAFUNZI WATAKA ELIMU YA AFYA MASHULENI


Leo Agosti 8, 2025 wanafunzi kutoka Wella Sekondari, Msalato na Jamhuri High School wametembelea Banda la Wizara ya Afya kwenye Maonesho yanayoendelea Viwanja vya Nzuguni, Dodoma. Ziara hiyo imekuwa fursa ya pekee kwao kupata maarifa kuhusu masuala mbalimbali ya afya na kueleza matarajio yao kwa taifa la kesho.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wanafunzi hao akiwepo, Saviola Gabriel wa Wella Sekondari wamesema Elimu ya afya ikiwemo masuala ya TB, VVU na lishe bora ikiwafikia shuleni, itawasaidia kulinda afya zao na kuwa mabalozi kwa jamii."

Saviola anaamini kwamba, elimu ya afya ikitolewa shuleni mapema, inawawezesha vijana kujikinga dhidi ya magonjwa na kuwa walinzi wa afya si tu kwao binafsi, bali pia kwa familia na marafiki.

Kwa upande wake Daniel Mnyinga kutoka Jamhuri High School amesema wanapaswa kufundishwa kuhusu homa ya ini, afya ya uzazi na malaria ili wawe na uelewa wa jinsi ya kujikinga na kusaidia wengine."

Kauli ya Daniel inasisitiza kuwa elimu ya afya mashuleni si kwa ajili ya kujilinda peke yake, bali pia na kuisaidia jamii kwa mapana zaidi.

 "maarifa haya yatatusaidia kutoa msaada wa haraka na sahihi pale changamoto za kiafya zinapotokea" amesisitiza Daniel.

Naye Faudhia Hamis anayesoma Msalato Sekondari amesema taifa lazima litambue kesho ya vijana wao.

"Sisi ni taifa la kesho, bila afya hatuwezi kufanikisha ndoto zetu,  tunaomba elimu hii iwe sehemu ya masomo shuleni kwetu," amesema Faudhia.

Faudhia anaona afya kama msingi wa kufanikisha malengo na ndoto za maisha. Kwa maoni yake, elimu ya afya ikijumuishwa kwenye mtaala wa shule itasaidia kujenga kizazi chenye mwamko wa kulinda afya zao.

Wanafunzi hao wamesisitiza kwa kauli moja kuwa, elimu ya afya inapaswa kufika shuleni ili kuhakikisha kizazi cha sasa kinakuwa na uelewa, kinga na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa kwa afya njema.

Awali watoa Elimu katika banda hilo la Afya akiwepo Atley Kuni wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Afya, Bi. Ester Ntulo Afisa Mpango wa Kudhibiti UKIMWI na Magonjwa yakuambukiza, waliwatahadharisha wanafunzi hao kutojihusisha na ngono wakiwa shuleni ili watimize ndoto zao. 

Post a Comment

0 Comments