Uamuzi huo umetangazwa jijini Dodoma na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Omar Shaban, mara baada ya Mpina na mgombea mwenza wake, Fatma Fereji, kuthibitishwa rasmi na INEC kugombea nafasi ya urais na makamu wa rais.
Akitangaza uamuzi wa Tume, Mwenyekiti wa INEC, Jaji mstaafu Jacobs Mwambegele, alisema kuwa kila mgombea wa urais atapatiwa gari jipya pamoja na dereva kwa ajili ya shughuli za kampeni. Hata hivyo, mara baada ya kauli hiyo, Omar Shaban alisimama na kueleza msimamo wa chama:
> “Tunashukuru kwa heshima hii, lakini tumeelezwa na kamati kuu ya chama kusisitiza kwamba tuna rasilimali zetu za magari. Tumeamua gari hilo litumike kwa matumizi mengine ya uchaguzi, si kwa mgombea wetu,” alisema Shaban.
Kwa msimamo huo, ACT Wazalendo imepinga utaratibu uliozoeleka ambapo wagombea wengine 17, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan wa CCM, walikabidhiwa magari mapya tangu Agosti 27, 2025.
Kesi Mahakamani
Tukio hilo linakuja siku chache baada ya ACT Wazalendo kushinda kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dodoma, kufuatia uamuzi wa awali wa INEC kumzuia Mpina kuwasilisha fomu za kugombea urais.
Jopo la majaji watatu—Abdi Kagomba (Kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa na John Kahyoza—lilitoa hukumu Septemba 11, 2025 likibatilisha uamuzi wa INEC na kuiruhusu ACT kuendelea na mchakato wa uchaguzi. Mahakama ilibainisha kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa Katiba, ikiwemo kutopewa haki ya kusikilizwa kwa walalamikaji.
Uzinduzi wa Kampeni Pemba
Wakati hali hiyo ikiendelea, chama hicho kimezindua rasmi kampeni zake za uchaguzi Zanzibar katika uwanja wa Tibirinzi, Chake Chake, Pemba. Tukio hilo limehudhuriwa na maelfu ya wanachama, ambapo mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT, Othman Masoud Othman, alikuwa mgeni rasmi.
Akihutubia hadhara hiyo, aliyekuwa kiongozi mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, alimuelezea Othman kama “lulu ya Zanzibar” akisisitiza kuwa ndiye kiongozi pekee anayeweza kuendeleza ndoto na misingi ya marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.
> “Nimemfahamu Othman kwa muda mrefu. Ni kiongozi thabiti, mwenye msimamo na jasiri kupigania heshima ya Zanzibar. Huyu ndiye mwendelezo wa ndoto za Maalim Seif,” alisema Zitto huku akishangiliwa na maelfu ya wafuasi.
Kwa mujibu wa Zitto, chini ya uongozi wa Othman Masoud, Zanzibar itarudisha hadhi yake, kuimarisha uchumi na kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali zao.

0 Comments