Header Ads Widget

Dk. Samia Aahidi Kituo cha Kumbukumbu cha Muungano

 



Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeimarika na sasa umekuwa wa undugu wa damu, huku akiahidi kuanzisha kituo cha kumbukumbu na nyaraka za muungano huo.


Akihutubia maelfu ya wananchi wa Kusini Unguja leo, Septemba 17, 2025, Dk. Samia alisema Muungano huo umeendelea kulinda uhuru na mapinduzi ya Zanzibar, na ni nguzo muhimu ya amani na mshikamano wa Taifa.


> “Tumedumisha umoja, amani na utulivu nchini. Hizi ndizo tunu za msingi za maendeleo ya Taifa letu. Kwa juhudi kubwa tunawahakikishia kuendelea kulinda muungano, umoja na amani ya nchi yetu,” alisema.



Aliongeza kuwa tunu hizo zimeifanya Tanzania kuwa na utambulisho wa kipekee kimataifa, ikijipatia nafasi kubwa ya ushirikiano wa kidiplomasia na kuwa mbia muhimu anayetegemewa duniani.


Aidha, Dk. Samia aliahidi kuanzisha Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kitakachosaidia vizazi vya sasa na vijavyo kuelewa historia na thamani ya muungano huo.


> “Tutaunda kituo cha kumbukumbu ili vijana wetu na wageni wajifunze maana ya muungano, ulivyoundwa na jinsi unavyoendelezwa,” alisisitiza.



Kuhusu maendeleo, alisema wananchi wengi walioshiriki mkutano huo walieleza kuridhishwa na kazi zilizotekelezwa katika kipindi cha uongozi wake.


> “Kwa bahati nzuri wamesema hawana deni na hawatudai. Wapo tayari kutupa nafasi nyingine tuendelee kuwaletea maendeleo zaidi. Ndugu zangu, maendeleo ni hatua, kila awamu inafanya sehemu yake na nyingine kuendeleza,” alisema Dk. Samia.


Alimalizia kwa kushukuru Watanzania kwa ushirikiano waliompa katika miaka mitano iliyopita, akiahidi kuendeleza kazi kubwa zilizofanyika endapo atapewa nafasi nyingine.

Post a Comment

0 Comments