Header Ads Widget

Maafisa wa FERWAFA Wazuiliwa kwa Uchunguzi wa Makosa ya Fedha

 


Ofisi ya Upelelezi wa Taifa ya Rwanda (RIB) imethibitisha kuwa inawachunguza maafisa wawili wa Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA) kwa makosa ya uhalifu ikiwemo utakatishaji fedha na ubadhirifu.


Maafisa hao ni Adolphe Kalisa, maarufu kwa jina la Camarade, ambaye amekuwa Katibu Mkuu wa FERWAFA tangu mwaka 2023, pamoja na Eric Tuyisenge, aliyewahi kuwa msimamizi wa vifaa vya timu ya taifa ya Rwanda, Amavubi.


Kwa mujibu wa taarifa ya RIB, uchunguzi huo umefanywa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi la Rwanda, na tayari wawili hao wamefunguliwa mashtaka yanayohusiana na ufisadi, matumizi ya hati ghushi na ubadhirifu wa mali za umma.


RIB imesema kuwa faili la Adolphe Kalisa tayari limewasilishwa kwa upande wa mashtaka ili hatua za kisheria ziweze kuendelea. Hata hivyo, Kalisa na Tuyisenge bado hawajatoa maelezo yoyote hadharani kuhusu tuhuma zinazowakabili.


Kwa sasa washukiwa hao wanashikiliwa katika vituo vya polisi vya Remera na Kicukiro, jijini Kigali.


Ingawa makosa kamili bado hayajawekwa wazi, taarifa kutoka vyombo vya habari nchini Rwanda zinaeleza kuwa kashfa hiyo huenda inahusiana na matumizi mabaya ya fedha za bajeti ya timu ya taifa wakati wa michezo ya kimataifa.


Shirikisho la Soka la Rwanda limekuwa likipitia mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi, huku mara kwa mara likikumbwa na malalamiko kuhusu ukosefu wa uwazi katika usimamizi wa fedha.

Post a Comment

0 Comments