Header Ads Widget

Dk. Nchimbi Awasili Ruvuma Kuendelea na Kampeni za CCM

 


Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, amewasili leo, Septemba 19, 2025, mjini Songea mkoani Ruvuma kuendelea na harakati za kampeni za chama hicho.


Dk. Nchimbi anatarajiwa kuungana kesho na Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye naye atawasili mkoani humo. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa wawili hao kushiriki kampeni katika mkoa mmoja tangu Agosti 28, 2025, walipozindua rasmi kampeni za kitaifa jijini Dar es Salaam.


Mara baada ya uzinduzi huo, viongozi hao waligawana majukumu ya kunadi Ilani ya CCM na kueleza mafanikio ya miaka mitano iliyopita pamoja na mipango ya miaka ijayo endapo watachaguliwa kuendelea kuongoza nchi.


Dk. Samia alianza kampeni zake katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe, Iringa, Singida, Tabora, Kigoma pamoja na mikoa mitatu ya Zanzibar ikiwemo Kusini Unguja, Kaskazini Unguja na Kusini Pemba.


Kwa upande wake, Dk. Nchimbi alianza safari yake ya kisiasa kupitia Kanda ya Ziwa akipita katika mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita na Kagera, kisha kuelekea Rukwa, Katavi, Arusha, Kilimanjaro na Tanga. Safari hiyo sasa inamrejesha nyumbani, Ruvuma, ambako anatarajiwa kupata mapokezi makubwa kutoka kwa wananchi wa mkoa huo.

Post a Comment

0 Comments