Header Ads Widget

Yanga Yaitungua Wiliete 3-0, Yaweka Mguu Raundi ya Pili Ligi ya Mabingwa

 


Klabu ya Yanga SC imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa Wiliete De Benguela ya Angola kwa mabao 3-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa Ijumaa, Septemba 19, 2025.


Mabao ya Wanajangwani yalifungwa na Aziz Andabwile dakika ya 32, Edmund John dakika ya 72 na Prince Dube aliyekamilisha karamu ya mabao dakika ya 81. Ushindi huo unaipa Yanga nafasi kubwa ya kufuzu kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa wiki ijayo jijini Dar es Salaam.


Kwa matokeo haya, Yanga inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare nyumbani ili kusonga mbele. Hata wakipoteza kwa tofauti ya mabao mawili au moja, bado watasalia na nafasi ya kufuzu kutokana na faida ya ushindi mnono wa ugenini.


Katika mchezo huo, kocha wa Yanga alifanya mabadiliko machache kwenye kikosi chake ikilinganishwa na kile kilichocheza dhidi ya Simba SC kwenye Ngao ya Jamii, ambapo Bakari Mwamnyeto, Mamadou Doumbia na Clement Mzize walipata nafasi ya kuanza.


Huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa Yanga msimu huu bila kuruhusu bao, baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba katika Ngao ya Jamii. Endapo itafuzu, Yanga itakutana na mshindi kati ya Elgeco Plus ya Madagascar na Silver Strikers ya Malawi katika raundi inayofuata.

Post a Comment

0 Comments