Simba SC leo inaanza rasmi kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kukutana na Gaborone United ya Botswana, katika dimba la Obedi Itani Chilume, Francistown, mchezo ukitarajiwa kuanza saa 2:00 usiku.
Wekundu wa Msimbazi wanaingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu njema barani Botswana, kwani katika historia yao hawajawahi kupoteza mchezo wowote katika ardhi hiyo. Katika michezo mitatu waliyocheza huko nyuma, Simba iliwahi kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Botswana Defence Force mwaka 2003, ikashinda 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy mwaka 2021, na mwaka 2023 ikatoka sare ya bila kufungana na Jwaneng Galaxy.
Historia pia inaweka rekodi nzuri kwa klabu nyingine za Tanzania nchini Botswana, ambapo Yanga SC na Mtibwa Sugar waliwahi kurejea na matokeo chanya, jambo linaloongeza imani kwa Simba kuelekea pambano la leo.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, akizungumza kabla ya mtanange huo, amesisitiza kuwa timu yake imejiandaa kwa umakini mkubwa, ikilenga kusonga mbele hadi hatua ya makundi. “Tumepata mazoezi mazuri kupitia Ngao ya Jamii na Simba Day. Lengo letu ni kushinda nyumbani na ugenini, lakini bado tunaiheshimu Gaborone United kama mabingwa wa nchi yao,” alisema Davids.
Kwa mujibu wa ratiba ya CAF, mshindi wa mchuano huu atakutana na mshindi kati ya Simba Bhora ya Zimbabwe na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, hatua itakayoweka picha kamili ya safari ya Simba katika kuwania kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

0 Comments