Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameendelea na ziara yake ya kampeni Kanda ya Kaskazini, akihutubia mamia ya wananchi katika uwanja wa Mashujaa, Moshi mjini, mkoa wa Kilimanjaro leo, Jumamosi Septemba 13, 2025.
Dkt. Nchimbi, ambaye ni mgombea mwenza wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokelewa kwa shangwe kubwa kabla ya kuwataka wananchi wa Kilimanjaro kuwapa kura za kishindo wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani.
Katika hotuba yake, alitumia nafasi hiyo kumtambulisha Ibrahim Mohamed Shayo, mgombea ubunge wa Moshi Mjini, pamoja na wagombea wengine wa ubunge na madiwani wa chama hicho mkoani humo.
Akizungumza kwa msisitizo, Dkt. Nchimbi alisema Ilani ya CCM ya uchaguzi wa mwaka 2025-2030 inalenga moja kwa moja katika kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza ustawi wa maendeleo na kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na rasilimali za nchi.
"Wananchi wa Kilimanjaro na Watanzania wote, tunasema sasa ni wakati wa kuimarisha safari ya maendeleo iliyoanzishwa na Dkt. Samia. Kupitia Ilani hii, tunalenga huduma bora zaidi za kijamii, fursa za ajira, na uchumi imara kwa kila familia," alisema Dkt. Nchimbi.
Kabla ya kuwasili Moshi, Dkt. Nchimbi alianza mikutano yake ya kampeni mkoani Arusha, na sasa akiendelea na mikoa mingine ya Kanda ya Kaskazini kusaka kura za ushindi wa kishindo kwa CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

0 Comments