Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameweka bayana dira yake ya kuimarisha maisha ya wafanyakazi wa serikali na walimu iwapo atachaguliwa kuongoza visiwa hivyo.
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika viwanja vya Tibirinzi, Chake Chake – Pemba, Othman alisema mabadiliko ya kweli kwa Zanzibar hayawezi kusubiri na lazima yaanze mara moja.
Kiongozi huyo aliahidi kuwa moja ya hatua za kwanza za serikali yake itakuwa kuhakikisha kila askari wa vikosi vya Usalama wa Mapinduzi Zanzibar (SMZ) anaanzia mshahara wa angalau shilingi milioni moja, akisisitiza kuwa hatua hiyo itawawezesha askari kuendesha maisha bora, kuimarisha familia zao na kuongeza morali ya kulitumikia taifa.
"Tunataka Zanzibar yenye usawa na inayowathamini watumishi wake. Walimu, askari na kila mfanyakazi wa serikali watapewa heshima na haki zao mara moja, kwa sababu wao ndio msingi wa maendeleo ya taifa letu," alisema Othman mbele ya maelfu ya wafuasi na wanachama wa ACT Wazalendo.
Kwa kauli hiyo, mgombea huyo amejikita kuonyesha dhamira ya kuijenga Zanzibar yenye uchumi imara, haki kwa watumishi wa umma na mazingira ya kazi yenye heshima kwa kila raia.

0 Comments